Pesa Zikaingia, Biggie Akatoeka: DCI Yaangazia Sakata La KSh43,320
Kosa la tarakimu moja katika kutuma pesa kwa njia ya simu limegeuka kuwa mwanzo wa sakata la kutoweka kwa mshukiwa, huku aliyepokea fedha akidaiwa kuzima simu, kutoa SIM kadi na kutoweka kusikojulikana aliko.
Katika ujumbe wa kejeli uliojaa tahadhari kuhusu ulaghai wa kifedha, Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) imeangazia kisa cha mwanamume anayejulikana kwa jina la utani ‘Biggie wa Deals’, ambaye anadaiwa kupokea KSh43,320 kimakosa kabla ya kutoweka.
Kwa mujibu wa DCI, tukio hilo lilitokea Alhamisi iliyopita wakati mfanyabiashara mmoja, Zack, alipokuwa akijaribu kutuma fedha hizo kwa msambazaji wake ili kulipia bidhaa zilizokuwa zikihitajika haraka.
Hata hivyo, kosa la tarakimu moja lilifanya pesa hizo kuingia katika akaunti ya simu ya Biggie, ambaye anadaiwa kuwa mhustler anayefahamika katika eneo analoishi.
Baada ya kupokea ujumbe wa muamala, Biggie alidaiwa kukagua salio lake mara kadhaa, huku akionekana kutambua kuwa fedha hizo hazikuwa zake.
Awali, aliripotiwa kufikiria kurejesha pesa hizo kwa mwenyewe, lakini baadaye akabadilisha msimamo na kuanza kupanga namna ya kuzitumia.
DCI inadai kuwa ndani ya dakika chache, Biggie alizima simu yake, akaondoa SIM kadi na kutoweka katika makazi yake ya kawaida, huku shughuli zake za jioni zikihamishwa hadi eneo lisilojulikana.
Hali hiyo ilimwacha Zack akijaribu kumpigia simu bila mafanikio, huku mwenye nyumba wa Biggie naye akibaki na maswali baada ya mpangaji huyo kutoweka akiwa na deni la kodi ya miezi miwili.
Kwa mujibu wa ujumbe huo, Biggie alikuwa ameambatanisha malipo yake ya mwisho ya kodi na ujumbe wa kumtaka mwenye nyumba kuweka kufuli kwenye nyumba hiyo.
DCI imetumia kisa hicho kuonya dhidi ya tabia ya kupokea pesa kimakosa na kuzitumia au kutoweka badala ya kuzirejesha kwa mwenyewe.
Idara hiyo imesisitiza kuwa kupokea pesa za mtu mwingine na kuamua kuzihifadhi kunaweza kugeuka kuwa kosa la jinai, licha ya fedha hizo kuingia kwenye akaunti kwa bahati mbaya.
Visa sawa na hiki vimekuwa vikiripotiwa mara kwa mara nchini.









