Huku mataifa yaliyoendelea yakizidi kuimarisha mikakati ya kukabiliana na uhalifu wa kimtandao, wahalifu wanaotumia teknolojia ya kisasa wameendelea kubuni mbinu mpya za kuiba fedha, huku shambulio dhidi ya Binance likidhihirisha ukubwa wa tishio hilo katika sekta ya fedha za kidijitali.
Wateja wa Binance, jukwaa kubwa zaidi duniani la biashara ya sarafu za kidijitali, wameondoa mali yenye thamani ya dola bilioni 3.64, sawa na takriban KSh473 bilioni, baada ya kampuni hiyo kurejesha huduma za kutoa fedha Jumapili kufuatia shambulio la kihistoria lililoathiri mali za kidijitali zenye thamani ya dola bilioni 6.3, takriban KSh819 bilioni.
Uondoaji huo mkubwa wa fedha umeibua maswali kuhusu usalama wa uwekezaji katika majukwaa ya sarafu za kidijitali, huku wateja wakionekana kuchukua tahadhari baada ya taarifa za shambulio hilo kusambaa.
Binance ilikuwa imesimamisha kwa muda huduma za kutoa fedha kufuatia tukio hilo, kabla ya kurejesha miamala kwa awamu huku ikiahidi kufidia hasara iliyotokana na wizi huo.
Kampuni hiyo imesema imeweza kurejesha au kununua upya takriban asilimia 95 ya mali zilizoibwa, huku ikiahidi kugharamia hasara iliyosalia bila kuwapa wateja mzigo wa kifedha.
Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) limehusisha shambulio hilo na Korea Kaskazini, likilitaja kundi la wahalifu wa mtandao linalojulikana kama TraderTraitor.
Kundi hilo pia linahusishwa na wizi wa dola bilioni 1.5 kutoka jukwaa la Bybit mwaka 2025, tukio lililoonyesha namna mashambulizi ya kimtandao yanavyoweza kuathiri mifumo mikubwa ya kifedha duniani.
Wizi huo wa Binance unaongeza orodha ya mashambulizi makubwa dhidi ya majukwaa ya sarafu za kidijitali, huku wataalamu wakionya kuwa mifumo ya kifedha inayotegemea teknolojia inahitaji ulinzi wa hali ya juu zaidi.
Mwaka 2025, takriban dola bilioni 2.9 za sarafu za kidijitali ziliibwa katika matukio karibu 150 ya uhalifu wa mtandao, hali inayoonyesha ukubwa wa changamoto inayokabili sekta hiyo.
Huku wizi huo ukizidi kuongezeka, usalama wa mifumo ya kifedha ya kidijitali na imani ya wateja vinaendelea kuwa changamoto kubwa kwa kampuni za teknolojia na serikali duniani huku mikakati zaidi,ikiandaliwa.









