Aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i amekosoa vikali hatua ya raia wa kigeni wanaokamatwa nchini Kenya na baadaye kupelekwa katika mataifa yao bila kufuata taratibu za kisheria, akitumia kisa cha mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda, Dkt Kizza Besigye, kuelezea wasiwasi wake.
Matiang’i amesema hakuna raia wa kigeni anayepaswa kukamatwa nchini Kenya na kukabidhiwa kwa serikali ya nchi yake kwa namna ambayo Besigye aliondolewa nchini, akitaja tukio hilo kuwa lisilokubalika.
Akizungumza kuhusu suala hilo,
Matiang’i alisema: “Hakuna raia wa kigeni atakayekamatwa nchini Kenya na kukabidhiwa kwa nchi yake kwa namna ambayo Kizza Besigye alivyofanyiwa. Hilo si sawa kabisa.”
Kauli hiyo inaibua tena mjadala kuhusu wajibu wa Kenya katika kulinda haki za watu wanaoishi au kutembelea nchini, wakiwemo raia wa mataifa mengine, hasa wanapokabiliwa na mashtaka katika nchi zao.
Besigye, ambaye amekuwa mpinzani wa muda mrefu wa Rais wa Uganda Yoweri Museveni, alitoweka jijini Nairobi Novemba 16, 2024, alipokuwa ametembelea Kenya kuhudhuria uzinduzi wa kitabu.
Siku nne baadaye, alionekana katika mahakama ya kijeshi jijini Kampala, Uganda, akiwa pamoja na mshirika wake Haji Obeid Lutale
Tukio hilo lilizua maswali kuhusu namna alivyotoka Kenya na kupelekwa Uganda, huku madai yakitolewa kuwa alitekwa na kuhamishwa kwa lazima bila kufuata utaratibu wa kawaida wa kumrejesha mshukiwa katika nchi inayomtaka.
Baada ya tukio hilo, serikali ya Kenya ilisema ilikuwa ikichunguza mazingira ya kutoweka kwa Besigye, huku maafisa wa Uganda wakidai kuwa operesheni ya kumkamata ilifanyika kwa ushirikiano kati ya vyombo vya usalama vya mataifa hayo mawili.
Besigye na Lutale baadaye walifikishwa mbele ya mahakama ya kijeshi nchini Uganda na kushtakiwa kwa makosa yanayohusiana na usalama na umiliki wa silaha kinyume cha sheria.
Tukio hilo lilizua mjadala kuhusu taratibu za kisheria zinazopaswa kufuatwa katika kurejesha washukiwa wa uhalifu kutoka nchi moja kwenda nyingine.
Kwa mujibu wa taratibu za kurejesha washukiwa, maarufu kama extradition, nchi inayomtaka mshukiwa inapaswa kuanzisha mchakato rasmi, huku mahakama ya nchi alimokamatwa ikichunguza uhalali wa ombi hilo kabla ya uamuzi wa kumkabidhi.
Matiang’i, ambaye aliwahi kuhudumu katika wizara mbalimbali za serikali ya Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, sasa ni miongoni mwa wanasiasa wanaohusishwa na maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Kauli yake inaongeza mjadala kuhusu haki za binadamu, utawala wa sheria na namna Kenya inavyopaswa kushughulikia masuala ya usalama yanayohusisha mataifa jirani.









