Mchekeshaji maarufu wa Uganda, Yokana Mbuuse, anayefahamika kwa jina la kisanii Kapere Lufotose, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 56, na kuwaacha mashabiki wake katika majonzi.
Kapere alifariki Jumapili, Novemba 1, 2026, katika hospitali moja iliyoko Buddo, Wilaya ya Wakiso nchini Uganda.
Hata hivyo, chanzo rasmi cha kifo chake hakikuwa kimetangazwa kufikia wakati wa kuchapishwa kwa taarifa hizo.
Ripoti za vyombo vya habari vya Uganda zinasema Kapere alilalamikia maumivu makali ya kichwa kabla ya hali yake kudorora na kuhitaji huduma za hospitali.
Hata hivyo, haijathibitishwa rasmi kuwa maumivu hayo ndiyo yaliyosababisha kifo chake.
Menejimenti yake pia ilieleza kuwa hakuwa akifahamika kuwa na ugonjwa wowote uliokuwa ukimsumbua kabla ya kifo chake.
Habari za kifo chake zilitangazwa na mwanasiasa na kiongozi wa chama cha National Unity Platform (NUP), Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine, kupitia mtandao wa kijamii wa X.
Katika ujumbe wake, Bobi Wine alieleza kusikitishwa na kifo cha Kapere, akimtaja kama rafiki, ndugu na mwenza aliyekuwa na kipaji cha kuleta furaha hata katika nyakati ngumu.
Safari yake katika tasnia ya burudani
Kapere alipata umaarufu mkubwa kupitia kundi la vichekesho la Amarula Family, ambako alifanya kazi pamoja na Allan Mujuni, anayefahamika kama Amooti, na Nicholas Mpiirwe, maarufu kama Messe Bontwe
Alitambulika kwa ucheshi wake wa kipekee, miondoko ya kuchekesha na uwezo wa kutumia sura yake pamoja na ishara za mwili kuwachekesha mashabiki.
Umaarufu wake uliongezeka kupitia maonyesho ya jukwaani na vipindi vya televisheni. Pia alishiriki katika video za muziki, ikiwemo wimbo wa Bobi Wine uliopewa jina la Mr Money, ambako aliigiza tajiri aliyetumia mali na pesa kutafuta mapenzi.
Safari yake ya kuwa mchekeshaji haikuwa rahisi. Katika mahojiano ya awali, Kapere alisimulia namna alivyokumbana na changamoto za maisha tangu utotoni, ikiwemo kukatizwa kwa masomo kutokana na tatizo la ngiri.
Alipoteza mama yake akiwa mchanga na kulelewa na babu na nyanya yake. Baadaye alifanya kazi za vibarua katika maeneo ya ujenzi kabla ya kupata msaada wa matibabu.
Licha ya changamoto hizo, aliweza kujijengea jina katika tasnia ya burudani na kugeuza hali iliyokuwa ikimfanya adhihakiwe kuwa chanzo cha mafanikio yake.
Mbali na burudani, Kapere alikuwa akijihusisha na siasa za Uganda kupitia chama cha NUP, ambapo mwaka 2025 alionyesha nia ya kuwania nafasi ya udiwani katika eneo la Makindye.
Alikuwa ameoa Lydia Nakandi, anayefahamika pia kama Mama Trump, na walikuwa wamejenga familia pamoja.
Kifo chake kimeibua salamu za rambirambi kutoka kwa mashabiki, wanasiasa na wadau wa burudani nchini Uganda.
Mipango ya mazishi na maelezo zaidi kuhusu mazingira ya kifo chake yalikuwa bado hayajatangazwa rasmi.









