Aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua ametangaza kujiunga kwa Mbunge wa Runyenjes Eric Muchangi Karemba katika chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP), hatua inayotajwa kuimarisha ushawishi wa chama hicho katika Kaunti ya Embu.
Gachagua alisema Karemba alitembelea makazi yake ya Wamunyoro asubuhi ya leo, ambapo alimkaribisha rasmi katika DCP baada ya kujiondoa katika chama cha United Democratic Alliance (UDA).
Katika taarifa yake, Gachagua alisema mbunge huyo atashirikiana na Mbunge wa Mbeere Kusini Gitonga Mukunji kueneza ushawishi wa DCP katika maeneo mbalimbali ya Embu, huku chama kikijiandaa kwa uchaguzi mkuu wa 2027.
Alisema chama hicho kinalenga kushinda kiti cha ugavana, viti vya ubunge pamoja na wadi zote 20 za kaunti hiyo, akionyesha azma ya DCP kupanua ushawishi wake kisiasa katika eneo la Mlima Kenya.
"Tumemkaribisha Mbunge wa Runyenjes, Mheshimiwa Eric Muchangi Karemba, katika chama cha DCP baada ya kujiondoa UDA. Atajiunga na Mheshimiwa Gitonga Mukunji katika kukitangaza chama kote Kaunti ya Embu," alisema Gachagua.
Aidha, Gachagua alitangaza kuwa atatembelea eneo bunge la Runyenjes wiki ijayo kwa ajili ya kumtambulisha rasmi Karemba kwa wakazi wa eneo hilo, hatua inayotarajiwa kuashiria mwanzo wa kampeni za kuimarisha chama hicho mashinani.
Karemba ni miongoni mwa viongozi wanaohusishwa na siasa za Embu, ambapo mabadiliko ya misimamo ya kisiasa yanazidi kuangaziwa kuelekea uchaguzi mkuu ujao.
Kujiondoa kwake UDA na kujiunga na DCP kunajiri wakati ambapo vyama vya kisiasa vinaendelea kujipanga upya, vikilenga kujenga miungano na kupata uungwaji mkono katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Gachagua amekuwa akihimiza kuimarishwa kwa DCP kama jukwaa la kisiasa linalolenga kuwakilisha maslahi ya wananchi, akisisitiza kuwa chama hicho kina nafasi kubwa katika siasa za Kenya za sasa na zijazo.
Katika ujumbe wake, Gachagua alisisitiza kuwa DCP ni chama kinacholenga kuongoza kizazi cha sasa na kijacho, akisema kina uwezo wa kushindana katika uchaguzi ujao.
"DCP ni chama cha sasa na cha siku zijazo," alisema Gachagua, akionyesha matumaini yake kuhusu ukuaji wa chama hicho na nafasi yake katika siasa za Kenya.









