Msanii maarufu wa muziki wa R&B nchini Marekani, Ne-Yo, amegusa hisia za mashabiki wake baada ya kumwandikia binti yake, Madi, ujumbe wa upendo na fahari katika kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa, akieleza namna anavyofurahia kumuona akikua huku akitamani muda usiende kwa kasi na kumwondolea kumbukumbu za utoto wake.

Kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye mitandao ya kijamii, Ne-Yo alieleza kuwa amejawa na hisia zinazokinzana, akifurahia mwanaye kukua na kuwa mwanamke mwenye matumaini makubwa, lakini wakati huohuo akihuzunika kuona hatua hizo zikimfanya aachane taratibu na utoto wake.

Msanii huyo alisema anajivunia mwanamke ambaye binti yake anakuwa, lakini anakiri kuwa sehemu yake bado inatamani kuendelea kumuona kama mtoto mdogo aliyekuwa akimlea.

Alieleza kuwa ingawa anasubiri kwa hamu kuendelea na safari ya maisha pamoja na mwanaye akiwa katika hatua mpya ya ukuaji, kila anapomtazama ataendelea kumkumbuka mtoto mdogo aliyewahi kuwa.

"Moja ya baraka kubwa zaidi kuwahi kunipata katika maisha yangu ni nafasi ya kuwa baba yako. Nakupenda, Madi Muu," aliandika Ne-Yo katika ujumbe wake, akihitimisha kwa kumtakia binti yake siku njema ya kuzaliwa.

Ujumbe huo umedhihirisha upande mwingine wa maisha ya mwanamuziki huyo, ambaye mashabiki wengi humfahamu kupitia nyimbo za mapenzi, mahusiano na burudani, lakini pia ni baba anayethamini nafasi yake katika maisha ya watoto wake.

Safari ya Ne-Yo katika muziki ilianza nyuma ya pazia akiwa mtunzi wa nyimbo kabla ya kujijengea jina kama mwimbaji wa kimataifa.

Ne-Yo, ambaye jina lake halisi ni Shaffer Chimere Smith, alizaliwa Oktoba 18, 1979, katika jimbo la Arkansas, Marekani, na kukulia Las Vegas ambako alianza kukuza kipaji chake cha muziki akiwa kijana.

Umaarufu wake ulianza kushika kasi mwaka 2004 baada ya kuandika wimbo "Let Me Love You" ulioimbwa na Mario, uliokuwa miongoni mwa nyimbo zilizotikisa chati za muziki duniani.

Mwaka 2006 alijitosa rasmi katika muziki kama mwimbaji wa kujitegemea kupitia albamu yake ya kwanza In My Own Words, iliyomletea mafanikio makubwa kupitia kibao So Sick.

Miongoni mwa nyimbo zake zilizomjengea umaarufu ni Because of You, Miss Independent, Closer na Sexy Love. Pia ameshirikiana na mastaa wengine wakubwa, huku akihusika katika utunzi wa nyimbo kama Irreplaceable ya Beyoncé na Take a Bow ya Rihanna.

Mafanikio hayo yamemwezesha kushinda tuzo tatu za Grammy, huku akiendelea kujitanua katika uigizaji na shughuli nyingine za burudani.

Katika maisha yake binafsi, Ne-Yo ni baba wa watoto saba kutoka mahusiano tofauti, jambo linaloonyesha nafasi muhimu ya familia katika maisha yake nje ya jukwaa.

Ujumbe wake kwa Madi umeongeza sura ya kibinadamu kwa msanii huyo, ukionyesha kuwa licha ya umaarufu na mafanikio ya kimataifa, furaha ya kumuona mtoto akikua na changamoto ya kumuaga mtoto mdogo aliyemzoea ni hisia ambazo hata mastaa wakubwa hukabiliana nazo.