Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini Kenya wamewataka wanasiasa kudhibiti matamshi yao ya hadharani, wakionya kuwa kauli za uchochezi, matusi na lugha inayogawa wananchi zinatishia umoja wa kitaifa na amani kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Maaskofu hao wamesisitiza kuwa viongozi wa kisiasa wanapaswa kutumia majukwaa yao kuhamasisha maridhiano, mshikamano na maendeleo badala ya kuyatumia kuchochea uhasama miongoni mwa Wakenya.
Onyo hilo linakuja wakati hali ya kisiasa nchini Kenya ikiendelea kupata joto huku wanasiasa kutoka mirengo tofauti wakizidisha mashambulizi ya maneno dhidi ya wapinzani wao katika mikutano ya hadhara na majukwaa mengine ya kisiasa.
Maaskofu hao, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu Katoliki nchini (KCCB), Askofu Mkuu Maurice Muhatia, na makamu wake Askofu Mkuu Anthony Muheria, walitoa kauli hiyo Alhamisi, Novemba 12, 2026, walipokuwa wakizungumza na wanahabari katika Kituo cha John Cardinal Njue Pastoral Centre, Embu.
Walisema kuwa kampeni za kisiasa hazipaswi kuwa kisingizio cha viongozi kutumia lugha inayochochea migawanyiko, wakikumbusha kuwa amani iliyopo nchini inaweza kuvurugwa na maneno yasiyozingatia uwajibikaji.
Aidha, maaskofu hao walitangaza kupiga marufuku wanasiasa kutoa hotuba za kisiasa ndani ya makanisa yote ya Katoliki nchini, wakielekeza mapadre kuhakikisha agizo hilo linatekelezwa bila upendeleo.
Askofu Mkuu Muheria alisema maeneo ya ibada yanapaswa kubaki kuwa sehemu za sala, upendo na umoja, ambako Wakenya wenye misimamo tofauti ya kisiasa wanaweza kukutana bila kushinikizwa kuunga mkono upande wowote.
Alisema wanasiasa wanaotafuta uungwaji mkono wana majukwaa mengine wanayoweza kutumia, yakiwemo vyombo vya habari, mikutano ya hadhara na mikutano ya wananchi, badala ya kutumia madhabahu kutafuta kura.
Katika taarifa yao, viongozi hao wa Kanisa pia walielezea wasiwasi kuhusu visa vya utekaji nyara, watu kutoweka kwa lazima na vitisho dhidi ya wanaharakati, waandishi wa habari na mashirika ya kiraia.
Wamezitaka idara za usalama kutekeleza majukumu yao bila kuegemea upande wowote wa kisiasa, huku wakilaani vitendo vinavyokiuka uhuru wa kujieleza na kukusanyika unaolindwa na Katiba.
Kuhusu maandalizi ya uchaguzi mkuu wa 2027, maaskofu hao waliitaka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru, wa haki na wa kuaminika.
Walisema tume hiyo inapaswa kulinda uhuru wake dhidi ya shinikizo kutoka kwa wanasiasa na watu wenye ushawishi, huku ikijenga imani ya wananchi katika mchakato mzima wa uchaguzi.
Vijana pia walihimizwa kujitokeza kupata vitambulisho vya taifa na kujiandikisha kama wapiga kura, huku wakionywa kutokubali kutumiwa kufanya vurugu au vitendo vya kuvuruga uchaguzi kwa malipo.
Maaskofu hao waliwataka pia Wakenya kutathmini utendaji wa viongozi wao na kufanya maamuzi ya busara watakapopiga kura mwaka ujao.









