Rais wa Kenya William Ruto ametangaza mpango wa kuwapandisha vyeo walimu 50,000 katika mwaka huu wa fedha, huku serikali yake ikiweka Sh4 bilioni kwa ajili ya kutekeleza zoezi hilo linalolenga kuimarisha maslahi na maendeleo ya kitaaluma ya walimu nchini humo.
Ruto alitoa ahadi hiyo Alhamisi, Novemba 12, 2026, wakati akifunga mkutano wa mwaka wa Chama cha Wakuu wa Shule za Elimu ya Msingi na Sekondari (KECSHA), uliofanyika katika eneo la Nyali, Mombasa.
Alisema hatua hiyo itakuwa miongoni mwa zoezi kubwa zaidi la upandishaji vyeo kwa walimu kuwahi kufanyika ndani ya mwaka mmoja nchini Kenya.
Kwa mujibu wa Rais huyo, Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) na Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC) tayari zimeidhinisha miongozo mipya ya maendeleo ya taaluma ya walimu, baada ya makubaliano yaliyofikiwa kati ya TSC na vyama vya wafanyakazi wa sekta hiyo.
Mbali na suala la upandishaji vyeo, Ruto alirejea ahadi ya serikali kutenga asilimia 20 ya nyumba zinazojengwa kupitia mpango wa nyumba za gharama nafuu kwa ajili ya walimu, licha ya mpango huo kukumbwa na changamoto za kisheria baada ya mahakama kuubatilisha.
Aidha, alisema serikali inaendelea kuboresha huduma za matibabu kwa walimu kupitia Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA), akibainisha kuwa mpango wa bima ya matibabu ya walimu unahudumia wanachama 426,642 pamoja na wategemezi 887,358.
Alisema huduma hizo sasa zinapatikana katika vituo vya afya zaidi ya 4,000 nchini kote, huku kiwango cha bima ya kulazwa hospitalini kikifikia Sh3 milioni.
Katika hatua nyingine, Ruto aliahidi kuhakikisha fedha za kugharamia shughuli za shule zinatolewa kabla ya muhula mpya kuanza kuanzia mwaka 2027.
Alisema serikali tayari imetoa zaidi ya Sh86 bilioni kwa shule katika awamu tatu za Januari, Aprili na Agosti mwaka huu.
Rais huyo pia aliagiza Wizara ya Elimu kushirikiana na KECSHA kuandaa mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Elimu ya Msingi ndani ya siku 90, ili kuweka mfumo bora wa usimamizi, ajira na ufadhili wa shule za elimu jumuishi.
Wakati huohuo, alitangaza mpango wa kuajiri walimu wengine 20,000 mwezi Desemba, akisema serikali yake tayari imeajiri walimu 100,000 katika kipindi cha miaka minne.
Mkutano huo ulihudhuriwa na zaidi ya wakuu wa shule 15,000, huku viongozi wa vyama vya walimu wakisifu hatua zilizochukuliwa na serikali katika kuboresha sekta ya elimu.
Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu nchini Kenya (KNUT), Collins Oyuu, amepongeza serikali kwa kuongeza ajira za walimu na kuboresha mazingira ya kazi.
Mwenyekiti wa KECSHA, Fuad Ali, naye aliunga mkono mageuzi yanayoendelea katika sekta ya elimu, akisema miongozo mipya ya kupandishwa vyeo itasaidia kumaliza changamoto ya walimu kukwama katika madaraja yao kwa muda mrefu.









