Dunia inaelekea kukumbwa na ongezeko kubwa la joto litakaloweza kuongeza majanga ya kimazingira, baada ya juhudi za mataifa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kukwama kwa miaka mitano mfululizo, huku sera zilizopo zikionyesha kuwa wastani wa joto unaweza kuongezeka kwa nyuzi joto 2.7 ifikapo mwaka 2100.

Onyo hilo limetolewa katika ripoti mpya ya Climate Action Tracker iliyozinduliwa Novemba 12, 2026, wakati wa mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi COP31 unaofanyika Antalya, Uturuki, huku wataalamu wakizitaka serikali kuongeza kasi ya utekelezaji wa mikakati ya kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mwenendo wa sasa wa sera za tabianchi unaweka dunia katika hatari ya kushindwa kufikia malengo ya Mkataba wa Paris wa mwaka 2015, uliolenga kudhibiti ongezeko la wastani wa joto duniani kuwa chini ya nyuzi joto mbili na kuendelea kufanya juhudi za kulipunguza hadi nyuzi joto 1.5 ikilinganishwa na kipindi cha kabla ya viwanda.

Hata endapo mataifa yatatekeleza kikamilifu ahadi zao za kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi ifikapo mwaka 2030 na 2035, ripoti hiyo inakadiria ongezeko la joto kufikia nyuzi joto 2.6 ifikapo mwishoni mwa karne hii.

Wataalamu wanaonya kuwa kuvuka kiwango cha nyuzi joto 1.5 kunaweza kuongeza hatari ya majanga ya kimazingira, yakiwemo ukame mkali, mafuriko, mawimbi ya joto kali na kuongezeka kwa matukio ya hali mbaya ya hewa.

Ripoti hiyo imebainisha kuwa licha ya matumizi ya nishati jadidifu kama vile jua na upepo kuongezeka katika mataifa mbalimbali, mafanikio hayo yanakwamishwa na ongezeko la mahitaji ya nishati na uwekezaji unaoendelea katika miundombinu ya mafuta, gesi asilia na makaa ya mawe.

Hali hiyo inaonyesha kuwa mataifa bado yanakabiliwa na changamoto ya kusawazisha mahitaji yao ya nishati na wajibu wa kulinda mazingira dhidi ya ongezeko la gesi zinazochangia kuhifadhi joto katika angahewa.

Climate Action Tracker imezitaka serikali kuharakisha mabadiliko kutoka matumizi ya nishati za kisukuku na kuongeza uwekezaji katika nishati safi ili kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa.

Pia, imesisitiza umuhimu wa kupunguza uzalishaji wa methane, ambayo ni miongoni mwa gesi zinazochangia ongezeko la joto duniani, pamoja na kuchukua hatua za kukomesha ukataji na uharibifu wa misitu.

Misitu ina mchango mkubwa katika kufyonza hewa ukaa na kudhibiti uwiano wa gesi katika angahewa, hivyo uharibifu wake unazidisha changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

Mkutano wa COP31 unawakutanisha viongozi wa serikali, wanasayansi na wadau wa mazingira kujadili hatua za pamoja za kukabiliana na changamoto hiyo.

Hata hivyo, ripoti hiyo inaonyesha kuwa licha ya mikutano na ahadi mbalimbali za kimataifa, kasi ya utekelezaji wa hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi bado haitoshi kuzuia dunia kuelekea katika ongezeko kubwa la joto.