Viongozi wa makanisa katika Kaunti ya Kirinyaga nchini Kenya wameishutumu serikali ya kaunti hiyo kwa kuruhusu kuendelea kwa biashara ya pombe haramu na dawa za kulevya, wakisema vitendo hivyo vinaharibu familia na kuhatarisha mustakabali wa watoto na vijana.

Viongozi hao wamedai kuwa ongezeko la baa zinazouza pombe hatari katika maeneo ya makazi, pamoja na biashara ya dawa za kulevya, limechangia kuvunjika kwa familia, kuongezeka kwa watoto wa mitaani na kuacha shule kwa vijana.

Wakizungumza katika eneo la Ngurubani, katika Kanisa la Chrisco, viongozi hao wakiongozwa na Askofu Jane Muchiri wa Muungano wa Kiinjili wa Kenya (EAK), tawi la Kirinyaga, walisema kanisa liko tayari kushirikiana na yeyote anayepambana na biashara hiyo haramu.

Mwenyekiti wa Chama cha Ushauri Nasaha na Saikolojia cha Kaunti ya Kirinyaga, Kamau Muchira, alisema makanisa yataunga mkono operesheni za kufunga baa zinazouza pombe haramu na kutoa ushahidi mahakamani pale inapohitajika.

Alisema jamii imechoshwa na hali inayowafanya vijana kupoteza maisha na familia kukosa amani kutokana na matumizi ya vileo hatari na dawa za kulevya.

Viongozi hao pia waliikosoa serikali ya kaunti kwa kile walichokitaja kuwa ni kukusanya ushuru kutoka kwa baa huku ikiendelea kutoa leseni kwa biashara zinazodaiwa kuuza pombe hatari katika vijiji.

Mchungaji Dedan Gathara wa Grace Gospel Church alisema serikali ya kaunti inapaswa kutambua kuwa jukumu lake la kutoa leseni halipaswi kutumiwa kuruhusu biashara zinazohatarisha maisha ya wananchi.

Alionya kuwa makanisa hayatakubali serikali kuendelea kunufaika kifedha kutokana na biashara zinazohusishwa na vifo na uharibifu wa maisha ya vijana.

Askofu Muchiri alisema pombe haramu lazima ikomeshwe ili wanaume warejee kutekeleza majukumu yao ya kifamilia na wanawake waache kubeba mzigo wa kulea familia peke yao.

Viongozi hao walisema baadhi ya baba na wana hutumia mapato yao kununua pombe haramu badala ya kugharamia mahitaji ya nyumbani, hali inayowaacha wanawake na watoto katika umaskini.

Aidha, walihusisha matumizi ya dawa za kulevya na ongezeko la wizi, vurugu na vijana kuacha shule kutokana na kupoteza mwelekeo wa maisha.

Waliwataka wazazi kufuatilia mienendo ya watoto wao na kuripoti wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya badala ya kuwaficha kwa kuhofia aibu.

Katika masuala ya kisiasa, viongozi hao waliwahimiza wakazi kujiandikisha kama wapiga kura kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027, huku wakitaka vyama vya siasa kufanya uteuzi wa wagombea kwa njia ya haki.

Walionya wanasiasa dhidi ya kutumia pombe na dawa za kulevya kushawishi vijana wakati wa kampeni, wakisisitiza kuwa hawatampa kura kiongozi anayechochea vurugu na kuvuruga maisha ya vijana.