Aliyekuwa Waziri wa Utumishi wa Umma na Masuala ya Jinsia nchini Kenya, Aisha Jumwa, amerejea katika chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA), miezi mitatu baada ya kukihama kufuatia kutofautiana na viongozi wa chama hicho kuhusu azma yake ya kuwania ugavana wa Kaunti ya Kilifi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Jumwa alipokelewa rasmi na Rais William Ruto katika Ikulu ya Mombasa Alhamisi, Novemba 12, 2026, hatua iliyohitimisha kipindi cha takribani miezi mitatu cha kutengana kwake na chama hicho ambacho alikuwa miongoni mwa wanachama wake waasisi.

Katika hafla hiyo, Ruto alimkabidhi Jumwa kofia yenye nembo ya UDA, ishara iliyotafsiriwa kuwa kurejea kwake rasmi katika chama hicho, huku akieleza utayari wake wa kufanya kazi naye katika kuimarisha shughuli za kisiasa za chama katika eneo la Pwani na maeneo mengine nchini.

Kupitia taarifa yake, Rais alisema anatarajia kushirikiana na Jumwa kuendeleza ajenda ya mageuzi ya chama hicho katika eneo la Pwani na taifa kwa ujumla.

“Ninatarajia kufanya kazi naye kuendeleza ajenda ya mageuzi ya chama katika Pwani na kote nchini. Tumejizatiti kuwaunganisha viongozi na Wakenya katika maono yetu ya Kenya yenye umoja, ushirikishwaji na maendeleo,” alisema Ruto.

Hatua hiyo inajiri miezi michache baada ya Jumwa kutangaza kujiondoa UDA Julai 30, 2026, akidai kuwa alikuwa amekumbana na unyanyasaji, kudharauliwa na kutengwa ndani ya chama licha ya mchango wake katika kukijenga na kukipigia debe wakati wa uchaguzi mkuu wa 2022.

Wakati wa kutangaza uamuzi wake nyumbani kwake Kakuyuni, Malindi, Jumwa alisema alikuwa amefanya mashauriano ya kina na wananchi wa Kilifi kabla ya kuamua kuondoka katika chama hicho.

Alilalamikia pia kile alichokitaja kuwa juhudi za baadhi ya viongozi wa chama kudhoofisha azma yake ya kuwania kiti cha ugavana wa Kilifi, akidai kuwa hakukuwa na nafasi ya kutosha kwa matarajio yake ya kisiasa.

Jumwa alieleza kuwa hata majaribio yake ya kuwasilisha malalamiko yake kwa Rais Ruto hayakuwa na mafanikio, akidai kuwa wakati mmoja alifukuzwa katika lango la Ikulu alipokuwa akijaribu kuhudhuria mkutano wa viongozi wa Pwani na Rais.

Baada ya kuondoka UDA, Jumwa alianza kushirikiana na viongozi wa upinzani, akiwemo kiongozi wa chama cha Wiper Patriotic Front, Kalonzo Musyoka, aliyemtembelea nyumbani kwake Agosti 14.

Kalonzo alimkaribisha katika Wiper na kupendekeza jina lake kwa nafasi ya naibu kiongozi wa chama hicho, huku akimuunga mkono katika azma yake ya kuwania ugavana wa Kilifi kupitia chama hicho.

Jumwa pia alitangaza kuunga mkono vuguvugu la kutaka Rais Ruto ahudumu kwa muhula mmoja, akiwataka wafuasi wake waliokuwa wamejiandikisha UDA kujiunga na Wiper.

Hata hivyo, kurejea kwake UDA kunafungua ukurasa mpya wa kisiasa huku mvutano kuhusu mgombea wa chama hicho katika kinyang'anyiro cha ugavana Kilifi ukiendelea kuangaziwa kuelekea uchaguzi wa 2027.

Jumwa aliwahi kuwa Mwakilishi wa Wanawake wa Kilifi kati ya mwaka 2013 na 2017 kabla ya kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Malindi mwaka 2017.

Baadaye aliteuliwa katika Baraza la Mawaziri la Rais Ruto, akihudumu katika wizara mbalimbali hadi alipoondolewa Julai 2024.

Hadi sasa, taarifa ya Rais kuhusu kurejea kwa Jumwa haijaweka wazi iwapo amepewa nafasi mpya ndani ya uongozi wa chama au iwapo azma yake ya kuwania ugavana wa Kilifi imepata suluhu.