Mahakama Kuu jijini Nairobi imekataa kusitisha kwa muda mkutano wa kitaifa wa wajumbe wa vuguvugu la Linda Mwananchi, licha ya kuthibitisha kuwa rufaa inayopinga uamuzi ulioruhusu mkutano huo kufanyika inahitaji kushughulikiwa kwa dharura.
Jaji Wilfrida Okwany ameamuru wahusika wote katika kesi hiyo kufikishiwa nyaraka za maombi hayo haraka, huku akielekeza shauri hilo kurejea mahakamani Novemba 16, 2026, kwa njia ya mtandao kwa maelekezo zaidi au kusikilizwa kwa maombi hayo.
Hata hivyo, mahakama ilisema haiwezi kutoa amri za muda zilizoombwa na mlalamikaji kwa sasa kwa kuwa haijapokea nakala ya uamuzi wa Mahakama ya Kutatua Migogoro ya Vyama vya Siasa (PPDT) uliotolewa Novemba 12, 2026.
Katika maagizo yake, mahakama ilieleza kuwa kukosekana kwa uamuzi huo kunafanya isiwezekane kuchunguza hoja zilizotolewa katika rufaa hiyo kabla ya kutoa uamuzi kuhusu maombi ya dharura.
Rufaa hiyo iliwasilishwa na mwanachama wa chama hicho, Emmanuel Willyngtone Khamala, muda mfupi baada ya mahakama ya PPDT kuondoa kizuizi kilichokuwa kikikabili mkutano wa kitaifa wa wajumbe wa vuguvugu hilo linaloongozwa na Seneta wa Nairobi, Edwin Sifuna.
Khamala anaitaka Mahakama Kuu kutengua uamuzi huo akidai kuwa mahakama ya awali ilikosea kutupilia mbali malalamishi yake kuhusu maandalizi ya mkutano huo na maamuzi yaliyofanywa bila kuwashirikisha wanachama waliosajiliwa.
Miongoni mwa hoja anazopinga ni uamuzi ulioruhusu uongozi wa chama kubadilisha jina kutoka The Equitable Party na kuwa Linda Mwananchi Movement bila kushauriana na wanachama au kupata maoni yao.
Pia anapinga uhalali wa mchakato wa uteuzi wa wagombea uliofanywa na vuguvugu hilo Oktoba 30, 2026, akidai kuwa haukuzingatia taratibu zinazostahili.
Kupitia wakili wake Danstan Omari, Khamala anasisitiza kuwa wanachama wengi wa chama hicho wanaweza kunyimwa nafasi ya kushiriki katika maamuzi muhimu kuhusu uongozi, uchaguzi na uteuzi wa wagombea.
Katika kesi hiyo, Edwin Sifuna ametajwa kuwa mhusika mwenye maslahi, huku Kamati Kuu ya Kitaifa ya Equitable Party, Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi ya chama hicho, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Kamati ya Mawasiliano ya Vyama vya Siasa zikitajwa kuwa wadaiwa.
Khamala anaiomba mahakama kuruhusu rufaa yake, kutengua uamuzi wa PPDT na kutoa amri za muda za kusitisha mkutano huo wa kitaifa wa vuguvugu hilo.









