Shughuli za biashara, mawasiliano na huduma za kidijitali katika mataifa mbalimbali zimeathiriwa na hitilafu kubwa ya mifumo ya kampuni ya teknolojia ya Microsoft, ambayo imeendelea kusumbua watumiaji licha ya kampuni hiyo kutangaza hatua za kurejesha huduma zake kwa sehemu.
Hitilafu hiyo iliyokumba huduma mbalimbali za Microsoft 365, ikiwemo Outlook, Teams na Copilot, ilianza kuathiri maelfu ya watumiaji nchini Marekani kabla ya kusambaa hadi eneo la Asia-Pacific, ambako ilivuruga shughuli za kawaida za taasisi za serikali na kampuni binafsi.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa Novemba 13, 2026, kampuni hiyo ilisema ilikuwa imefanya marekebisho katika baadhi ya seva zilizoathirika, lakini hatua hizo hazikuwezesha kurejea kwa huduma kwa uthabiti unaotarajiwa.
Microsoft ilieleza kuwa imeona baadhi ya huduma zikianza kurejea katika maeneo ambako marekebisho yalifanyika, huku ikiendelea kuchunguza hatua nyingine za kuimarisha mifumo yake ya kiteknolojia.
Takwimu za tovuti ya Downdetector, inayofuatilia taarifa za hitilafu za huduma za mtandaoni, zilionyesha kuwa zaidi ya watumiaji 130,000 nchini Marekani waliripoti matatizo ya huduma ya Outlook katika kilele cha hitilafu hiyo siku ya Alhamisi, Novemba 12.
Miongoni mwa matatizo yaliyoripotiwa ni kushindwa kutuma na kupokea barua pepe, kufungua akaunti na kupata huduma mbalimbali zinazotegemea mifumo ya Microsoft.
Athari hizo pia ziliripotiwa nchini India, Australia na Japan, huku taasisi za serikali za Australia na Japan pamoja na Bunge la Marekani zikiwa miongoni mwa taasisi zilizokumbwa na changamoto hizo.
Kampuni za teknolojia ya akili bandia (AI), OpenAI na Anthropic, pia ziliripoti matatizo yaliyohusishwa na mifumo inayowaunganisha na huduma za Microsoft, hali iliyoathiri baadhi ya zana zao za kidijitali.
Aidha, mashirika ya ndege ya India, IndiGo na Akasa Air, yaliripoti kuathirika kwa huduma zake za usaidizi kwa wateja zinazotegemea barua pepe.
Nchini Taiwan, hitilafu hiyo iliathiri shughuli za usimamizi wa fedha katika baadhi ya kampuni za uwekezaji, bima na taasisi za kifedha, huku kampuni moja ikilazimika kusitisha mpango wa kurejesha fedha za hati fungani uliokuwa umepangwa.
Hata hivyo, Microsoft ilisema haikuwa na taarifa zinazoashiria kuwa hitilafu hiyo ilisababishwa na shambulizi la kimtandao.
Waziri wa Mambo ya Ndani na Usalama wa Mtandao wa Australia, Tony Burke, alisema kwa mujibu wa maelezo aliyopokea, Microsoft iliamini kuwa tatizo hilo halikutokana na shambulizi la kimtandao, bali huenda lilihusiana na hitilafu katika masasisho ya mifumo yake.
Wachambuzi wa masuala ya teknolojia na uwekezaji wameonya kuwa kukumbwa kwa Microsoft na hitilafu zinazojirudia kunaweza kuibua maswali kuhusu uaminifu wa huduma zake, hasa kwa kampuni zinazotegemea mifumo hiyo kuendesha shughuli muhimu.
Tukio hilo ni la pili kuathiri huduma za Microsoft 365 mwaka huu, baada ya hitilafu nyingine kuripotiwa Januari, huku huduma yake ya Azure pia ikikumbwa na changamoto mwezi uliopita.









