Shauku ya kucheza mchezo mpya wa video wa Grand Theft Auto VI (GTA 6) imezua wasiwasi miongoni mwa shule nchini Uingereza, huku baadhi ya taasisi za elimu zikitoa maonyo kwa wazazi na wanafunzi dhidi ya kukosa masomo siku ya uzinduzi wa mchezo huo.
Shule hizo zimeonya kuwa kutohudhuria masomo kwa kisingizio cha kutaka kucheza mchezo huo hakutakubalika, na kutakuwa kukiuka taratibu za mahudhurio zinazotakiwa kufuatwa na wanafunzi.
Onyo hilo linatolewa wakati mchezo huo unaotarajiwa kuvutia mamilioni ya wachezaji ukitarajiwa kuzinduliwa nchini Uingereza Alhamisi, Novemba 19, 2026, hali inayozua hofu kuwa baadhi ya wanafunzi wanaweza kujifanya wagonjwa ili kubaki nyumbani na kupata nafasi ya kucheza GTA 6.
Hali hiyo imepewa jina la utani la 'GTA Flu', likimaanisha kujifanya kuugua ili kukwepa majukumu ya shule na kupata nafasi ya kucheza mchezo huo.
Shule kadhaa zimetuma barua kwa wazazi na walezi zikiwakumbusha kuhakikisha watoto wao wanaendelea kuhudhuria vipindi kama kawaida, huku zikisisitiza kuwa kutaka kucheza michezo ya video au shughuli nyingine za burudani si sababu inayokubalika ya kukosa masomo.
Katika juhudi za kuhakikisha wanafunzi hawatoroki shule, baadhi ya taasisi zimeanzisha motisha mbalimbali. Shule ya Ninestiles Academy iliyoko Birmingham imepanga kutumia basi dogo kuwafuata wanafunzi wanaokosa kufika shuleni na kuwarudisha madarasani.
Aidha, shule hiyo imeanzisha droo ya zawadi za vocha kwa wanafunzi watakaohudhuria masomo kwa siku zote za wiki husika.
Shule ya St John's Catholic School and Sixth Form College iliyoko Bishop Auckland nayo imetangaza droo ya zawadi ya vocha ya Amazon yenye thamani ya pauni 65 kwa wanafunzi watakaohudhuria masomo siku ya Alhamisi.
Wakati huo huo, shule ya Bradford Forster Academy imewataka wazazi kuhakikisha watoto wanazingatia muda wa kawaida wa kulala ili waweze kuamka mapema na kufika shuleni wakiwa wamepumzika.
Wazazi nchini Uingereza wanaweza kutozwa faini ya pauni 80 kwa kumruhusu mtoto kukosa shule bila sababu inayokubalika, huku kiasi hicho kikiongezeka hadi pauni 160 endapo hakitalipwa ndani ya siku 21. Katika mazingira mengine, hatua za kisheria zinaweza kuchukuliwa dhidi ya wazazi wanaoshindwa kuhakikisha watoto wao wanapata elimu.
Mchezo wa GTA 6 umetengenezwa na kampuni ya Rockstar Games na umepewa daraja la umri wa miaka 18 na kuendelea kutokana na maudhui yake ya watu wazima.
Mchezo huo ni mwendelezo wa GTA V iliyotolewa mwaka 2013, hivyo kuashiria kusubiri kwa takribani miaka 13 kwa mashabiki wa mfululizo huo.
Hofu ya shule hizo inaonyesha namna michezo ya video inavyoweza kuvutia vijana kiasi cha kuathiri shughuli zao za kila siku, huku taasisi za elimu zikijitahidi kuhakikisha burudani hiyo haiingilii masomo.









