Meli Mpya Yagonga Miamba,Serikali Yaunda Jopo Kuchunguza
Kufuatia kugonga miamba kwa meli mpya ya MV New Mwanza katika eneo la Bismarck ndani ya Ziwa Victoria, Serikali ya Tanzania imeunda timu maalum ya uchunguzi itakayobaini chanzo cha ajali hiyo pamoja na madhara yaliyotokana na tukio hilo.
Timu hiyo inayojumuisha wataalamu mbalimbali na vyombo vya usalama imepewa siku 14 kufanya uchunguzi wa kina na kutoa majibu ya kitaalamu kuhusu kilichosababisha meli hiyo kugonga miamba mapema asubuhi ya leo wakati ikifanya majaribio ya kawaida ya mifumo yake ndani ya Ziwa Victoria.
Taarifa hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Kamishna wa Polisi Salum Hamduni, ambaye amesema uchunguzi huo unalenga kubaini mazingira yote yaliyopelekea kutokea kwa ajali hiyo pamoja na kutathmini madhara yaliyosababishwa.
Hamduni amesema matokeo ya uchunguzi yatasaidia kufahamu chanzo cha hitilafu iliyosababisha meli hiyo kupata ajali, huku akisisitiza umuhimu wa kupata majibu ya kitaalamu kabla ya hatua nyingine kuchukuliwa.
Tukio hilo limezua taharuki miongoni mwa wakazi wa Mwanza, hususan wale waliokuwa karibu na eneo la Bismarck wakati meli hiyo ilipogonga miamba.
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo wameeleza namna walivyoshuhudia ajali hiyo kwa nyakati tofauti, huku wakiiomba Serikali kuhakikisha uchunguzi unafanyika kwa uwazi ili kubaini kilichotokea na kuzuia matukio kama hayo kujirudia.
Wakazi hao pia wameeleza umuhimu wa kuchukua hatua za kuhakikisha usalama wa vyombo vya majini, hasa vile vinavyotarajiwa kutoa huduma za kusafirisha abiria na mizigo katika Ziwa Victoria.
MV New Mwanza ni miongoni mwa miradi mikubwa ya usafiri wa majini nchini Tanzania, ikiwa imekamilika hivi karibuni na kuzinduliwa kwa gharama inayozidi shilingi bilioni 100.
Meli hiyo imekuwa ikifanyiwa majaribio ya kawaida ya mifumo yake kabla ya kuanza rasmi kutoa huduma za usafiri wa abiria na usafirishaji wa mizigo katika Ziwa Victoria.
Kuundwa kwa timu hiyo ya uchunguzi sasa kunatarajiwa kutoa ufafanuzi kuhusu hali ya meli hiyo na iwapo changamoto iliyojitokeza inaweza kuathiri mipango ya kuanza kwa huduma zake.
Hata hivyo,uchunguzi huo utatoa majibu









