Senegal imekumbwa na taharuki baada ya boti iliyokuwa imewabeba takribani wahamiaji 100 kuzama katika Bahari ya Atlantiki, huku makumi ya watu wakihofiwa kupoteza maisha na wengine kutoweka katika mkasa huo.

Tukio hilo limetokea karibu na eneo la Yenne, katika pwani ya Senegal, ambako juhudi za kutafuta manusura na miili ya watu waliopotea zinaendelea huku mamlaka zikikabiliana na ukubwa wa ajali hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa ya BBC, boti hiyo ilizama ikiwa na takribani watu 100 waliokuwa wakijaribu kusafiri kupitia bahari kuelekea Ulaya. Idadi kamili ya watu waliokuwa ndani ya chombo hicho na waliopatikana bado haijathibitishwa rasmi.

Taarifa za awali zilieleza kuwa mtu mmoja alikuwa amefariki dunia, huku baadhi ya vyombo vya habari vya ndani vikidai kuwa miili ya watu wengine ilikuwa imepatikana, ingawa idadi hiyo haikuwa imethibitishwa na mamlaka.

Serikali ya Senegal imeendelea kuratibu shughuli za uokoaji, huku taarifa zikieleza kuwa boti iliyoharibika ilifika ufukweni ikiwa na dalili za kuharibika vibaya. Vitu vya binafsi vya abiria vilipatikana ndani ya chombo hicho, hali iliyoongeza wasiwasi kuhusu idadi ya watu waliopotea.

Mwakilishi wa mkuu wa kijiji katika eneo hilo, Oumar Sow, alinukuliwa akisema kilio cha watu waliokuwa ndani ya boti hiyo kilisikika hadi ufukweni majira ya saa nane usiku, hali iliyoashiria ukubwa wa mkasa huo.

Taarifa za awali pia zinaeleza kuwa manusura mmoja aliyefanyiwa mahojiano na polisi alisema takribani watu 100 walikuwa ndani ya boti hiyo, wakiwemo wanawake na watoto.

Ajali hiyo imetokea ikiwa haijapita wiki mbili tangu mkasa mwingine wa aina hiyo kutokea nchini Senegal, ambapo angalau watu 39 walifariki dunia baada ya boti iliyokuwa imewabeba wahamiaji kuzama Novemba 8, 2026.

Boti hiyo ya mbao ilikuwa ikielekea Visiwa vya Canary nchini Hispania, kupitia njia ya Bahari ya Atlantiki inayotumiwa na maelfu ya wahamiaji kutoka Afrika Magharibi wanaotafuta fursa za maisha barani Ulaya.

Shirika la kutetea haki za wahamiaji la Walking Borders lilikadiria kuwa watu 635 walifariki katika njia hiyo kati ya Januari na Mei 2026 pekee.

Rais wa Senegal, Bassirou Diomaye Faye, amekuwa akionya kuhusu ongezeko la safari haramu za wahamiaji, huku akizitaka mamlaka kuimarisha mapambano dhidi ya mitandao inayopanga safari hizo hatari.

Serikali pia imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana, mojawapo ya sababu zinazotajwa kuchangia watu wengi kuamua kuhatarisha maisha yao wakitafuta maisha bora nje ya nchi.

Mamlaka za Senegal zinaendelea na juhudi za kutafuta waliopotea huku mkasa huo ukiibua tena mjadala kuhusu usalama wa safari za wahamiaji kupitia Bahari ya Atlantiki.