Rais William Ruto anatarajiwa kutumia ziara ya siku nane katika eneo la Magharibi mwa Kenya kueleza mafanikio ya serikali yake, kuimarisha ushawishi wa kisiasa na kuuza ajenda yake ya maendeleo kwa wananchi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027.
Ziara hiyo itakayohusisha kaunti za Busia, Bungoma, Kakamega na Vihiga, imegawanywa katika awamu mbili na itampa Rais fursa ya kukutana na wananchi, kuzindua miradi mipya pamoja na kukagua maendeleo ya miradi ambayo serikali yake ilianzisha awali.
Ziara hiyo inakuja wakati mazingira ya kisiasa nchini yakianza kupata joto kuelekea uchaguzi ujao, huku viongozi wa kisiasa wakiongeza mikakati ya kutafuta uungwaji mkono katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Katika awamu ya kwanza inayoanza leo, Ruto ataanza shughuli zake katika Kaunti ya Busia, ambako anatarajiwa kuzindua miradi kadhaa ya maendeleo ikiwemo jengo la ofisi katika Shule ya Msingi ya Kakemer.
Pia atazuru kambi ya jeshi ya Akichelesit na kuzindua jumba la utamaduni wa jamii ya Iteso katika eneo la Kakapel kabla ya kuanzisha ujenzi wa barabara ya Butula-Nambale-Amukura hadi Kocholia.
Baadaye Rais ataelekea Kaunti ya Bungoma, ambako atazindua ujenzi wa barabara ya Matisi-Bokoli-Milani-Teremi, kuanzisha ujenzi wa soko la Bokoli na shule ya mafunzo ya michezo katika eneo hilo kabla ya kuhutubia wananchi.
Siku ya Ijumaa, Rais atarejea Busia kwa shughuli nyingine za maendeleo, zikiwemo uzinduzi wa barabara ya Mau Mau Mabinju katika eneo bunge la Budalang’i na Shule ya Upili ya ACK Musoma.
Atazuru pia eneo bunge la Funyula kuanzisha ujenzi wa soko la Mulwanda kabla ya kuelekea Kakamega kwa shughuli zinazotarajiwa kufanyika katika maeneo ya Butere na Shinyalu.
Awamu ya pili ya ziara hiyo itaanza Novemba 28 katika eneo bunge la Butula, Busia, ambako Rais anatarajiwa kuzindua ujenzi wa mabweni katika Chuo cha Tiba cha Butula (KMTC), pamoja na mradi wa kuunganisha umeme katika makazi ya wananchi.
Baadaye ataelekea Misikhu katika Kaunti ya Bungoma na Navakholo pamoja na Ikolomani katika Kaunti ya Kakamega kwa uzinduzi wa miradi mingine.
Ziara hiyo itahitimishwa Desemba Mosi kwa shughuli katika maeneo ya Hamisi, Kaimosi, Shimanyiro, Lurambi na mji wa Kakamega katika Kaunti za Vihiga na Kakamega.
Huku miradi ya barabara, masoko, elimu na umeme ikiwa kiini cha ziara hiyo, macho pia yatakuwa kwa ujumbe wa kisiasa ambao Ruto atawasilisha kwa wakazi wa eneo hilo, hasa wakati kampeni za kujipanga kuelekea uchaguzi wa 2027 zikianza kushika kasi.









