Serikali ya Uingereza imechukua hatua ya kutaka kuzimwa kwa akaunti ya mwanahabari na mchekeshaji wa zamani Russell Brand kwenye mtandao wa YouTube, siku chache baada ya kupatikana na hatia ya ubakaji na unyanyasaji wa kingono na kuhukumiwa kifungo cha miaka 10 na nusu gerezani.
Kwa mujibu wa taarifa, Waziri wa Sheria nchini humo amekutana na wawakilishi wa kampuni ya Google, inayomiliki YouTube, na kuwasilisha ombi la kutaka akaunti ya Brand iondolewe kwenye jukwaa hilo.
Hatua hiyo inafuatia uamuzi wa kampuni ya Meta kuzifunga akaunti zake za Instagram na Facebook baada ya hukumu dhidi yake, huku serikali ikieleza wasiwasi kuhusu ujumbe alioweza kuwasilisha kwa umma akiwa gerezani.
Sakata hilo limechochewa zaidi na video iliyochapishwa kwenye akaunti yake ya YouTube mapema wiki hii, ambapo mkewe, Laura Brand, alisoma ujumbe aliodai kuupokea kutoka kwa mumewe.
Katika ujumbe huo, Brand alisisitiza kuwa hana hatia ya makosa yoyote ya kingono, licha ya mahakama kumpata na hatia na kumhukumu kifungo cha miaka 10 na nusu kwa kosa moja la ubakaji na makosa matatu ya unyanyasaji wa kingono.
Kufuatia kuchapishwa kwa video hiyo, Wizara ya Sheria imeanzisha uchunguzi kubaini iwapo Brand alikiuka kanuni za magereza zinazowazuia wafungwa kutoa taarifa za hadharani kupitia vyombo vya habari au njia nyingine bila kufuata taratibu zinazotakiwa.
Msemaji wa Waziri Mkuu Keir Starmer ameelezea kauli za Brand kuwa za kusikitisha na zisizokubalika, huku serikali ikitaka kuhakikisha maudhui yanayoweza kuwaumiza waathiriwa yanaondolewa.
Serikali pia imetaka YouTube kuondoa video hiyo maalum iliyochapishwa na mkewe Brand, ikisema maudhui hayo yanaweza kuongeza maumivu kwa watu walioathiriwa na makosa aliyopatikana nayo na hatia.
Msemaji wa serikali amesema ni jambo sahihi kuomba majukwaa ya kidijitali kuondoa maudhui yanayoweza kuumiza waathiriwa, ingawa uamuzi wa mwisho kuhusu kufuta maudhui hayo unabaki kwa kampuni husika kulingana na masharti yake.
Kwa upande mwingine, Google ilikuwa tayari imesimamisha uwezo wa Brand kupata mapato kupitia YouTube mwaka 2023, kufuatia madai ya ubakaji na unyanyasaji wa kingono yaliyoibuliwa dhidi yake kupitia uchunguzi wa vyombo vya habari.
Vyombo vya habari vimesema vimewasiliana na Google pamoja na Laura Brand ili kupata maoni yao kuhusu ombi la serikali.
Brand anatarajiwa kutumikia takribani miaka saba gerezani kutokana na hukumu hiyo ya miaka 10 na nusu.









