Benki ya Standard Chartered Kenya imeripoti ongezeko la asilimia 13 katika faida kabla ya kodi hadi kufikia Sh14.9 bilioni katika kipindi cha miezi tisa kilichokamilika Septemba 30, 2026, ikichochewa zaidi na ukuaji wa mapato yasiyotokana na riba.

Matokeo hayo yanaonyesha kuimarika kwa shughuli za benki hiyo licha ya kupungua kwa mapato ya jumla ya uendeshaji, hali iliyochangiwa kwa kiasi kikubwa na kushuka kwa mapato yatokanayo na riba katika mazingira ya viwango vya chini vya riba.

Akizungumza wakati wa kutangaza matokeo hayo, Afisa Mkuu Mtendaji na Mkuu wa Huduma kwa Wateja wa Benki hiyo, Birju Sanghrajka, alisema ukuaji huo umetokana na mikakati ya kuongeza mapato, kupanua huduma za kifedha na kuimarisha usimamizi wa gharama.

Sanghrajka alisema benki hiyo imeendelea kuwa na mwenendo mzuri wa biashara katika miezi tisa ya kwanza ya mwaka 2026, huku ikiimarisha uwezo wake wa kuwahudumia wateja na kusaidia malengo yao ya kifedha.

Kwa mujibu wa matokeo hayo, mapato yasiyotokana na riba yaliongezeka kwa asilimia 22 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita, yakichangiwa na ukuaji katika huduma za usimamizi wa utajiri na biashara za masoko ya fedha.

Hata hivyo, mapato yatokanayo na riba yalipungua kwa asilimia 18 kutokana na kubanwa kwa tofauti kati ya riba inayotozwa kwa mikopo na ile inayolipwa kwa amana, katika mazingira ya viwango vya chini vya riba.

Kwa ujumla, mapato ya uendeshaji yalipungua kwa asilimia sita, huku gharama za uendeshaji zikishuka kwa asilimia 14 kutokana na mikakati ya kudhibiti matumizi.

Aidha, fedha zilizotengwa kukabiliana na mikopo chechefu zilipungua kwa asilimia 62, hali iliyochangiwa na juhudi za kurejesha mikopo pamoja na kuimarika kwa ubora wa mali za benki hiyo.

Katika upande wa mikopo, salio la mikopo na malipo yaliyotolewa kwa wateja liliongezeka kwa asilimia 16 hadi kufikia Sh179.6 bilioni, ikilinganishwa na Desemba 2025.

Amana za wateja nazo ziliongezeka kwa asilimia 18 hadi Sh335 bilioni, huku mali zinazodhibitiwa kwa niaba ya wateja (AUM) zikikua kwa asilimia 19 hadi Sh361 bilioni.

Benki hiyo pia ilirekodi kuimarika kwa ubora wa mikopo yake, huku kiwango cha mikopo chechefu kikishuka kwa pointi 130 za msingi hadi asilimia 4.7.

Kwa upande wa ukwasi, benki iliripoti uwiano wa asilimia 61.75, zaidi ya kiwango cha chini cha kisheria cha asilimia 20, huku uwiano wa uwezo wa kukidhi mahitaji ya fedha za muda mfupi ukiwa asilimia 485 dhidi ya kiwango cha chini cha asilimia 100.

Sanghrajka alisema benki hiyo itaendelea kutekeleza mikakati yake ya ukuaji endelevu, huku ikifuatilia mabadiliko ya uchumi wa ndani na changamoto za kimataifa zinazoweza kuathiri biashara na masoko ya fedha.