Ndoto ya kuwa daktari imefikia tamati kwa Angel Wariaeli mwenye umri wa miaka 13, aliyepoteza maisha Novemba 18, 2026 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), zaidi ya mwaka mmoja baada ya kupigwa risasi wakati wa vurugu zilizotokea siku ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania Oktoba 29, 2025.

Kifo cha Angel kinaongeza kumbukumbu ya maumivu ya wananchi waliopoteza maisha na wengine kujeruhiwa katika machafuko yaliyoikumba Tanzania wakati na baada ya uchaguzi huo, ambapo mamia ya watu waliripotiwa kupata majeraha ya risasi na kuhitaji matibabu katika hospitali mbalimbali nchini.

Katika taarifa iliyotolewa Novemba 18, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa Muhimbili, Irene Charles Mbonde, alisema uongozi wa hospitali hiyo pamoja na familia ya marehemu wamepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Angel na kutoa pole kwa ndugu, jamaa na Watanzania wote walioguswa na msiba huo.

Angel alipigwa risasi begani Oktoba 29, 2025, majira ya saa tisa alasiri katika eneo la Manzese, Dar es Salaam, alipokuwa akimpelekea dada yake simu kwenye kibanda cha chakula cha familia yao.

Jeraha hilo lilisababisha madhara makubwa katika uti wake wa mgongo na kumfanya ashindwe kutembea, hali iliyomlazimu kukatiza masomo yake licha ya kuwa alikuwa amekamilisha darasa la saba na alikuwa na matarajio ya kuendelea na elimu ili kutimiza ndoto yake ya kuwa daktari.

Kwa kipindi chote cha kuugua, Angel alikabiliwa na changamoto za kiafya zikiwemo vidonda vilivyohitaji kusafishwa hospitalini kila Ijumaa, huku hali yake ikiendelea kuathiri maisha yake na familia yake.

Tukio lililompata Angel lilikuwa sehemu ya kipindi kigumu kilichoshuhudiwa nchini Tanzania wakati wa uchaguzi wa Oktoba 29, 2025, ambapo maandamano na makabiliano kati ya waandamanaji na vyombo vya usalama yaliripotiwa katika miji mbalimbali.

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu, Amnesty International, liliripoti kuwa wataalamu watatu wa afya katika hospitali za umma Dar es Salaam, Arusha na Mwanza walieleza kupokea mamia ya watu waliokuwa na majeraha ya risasi kati ya Oktoba 29 na 31, 2025. Waliojeruhiwa walijumuisha vijana, wanawake na watoto.

Kwa upande wake, Human Rights Watch ilisema uchunguzi wake kuhusu vurugu hizo ulibaini kuwa raia ambao hawakushiriki maandamano pia walipigwa risasi na kujeruhiwa, huku shirika hilo likitaka uwajibikaji kwa ukiukaji wa haki za binadamu.

Baada ya vyombo vya habari kuripoti mahangaiko ya Angel na mama yake Oktoba 31, 2026, alipata msaada uliomwezesha kupelekwa Muhimbili ambako madaktari bingwa walimuanza matibabu.

Hata hivyo, juhudi hizo hazikuweza kuokoa maisha yake, na sasa familia yake imepoteza mtoto aliyekuwa na ndoto ya kuokoa maisha ya wengine kupitia taaluma ya udaktari.