Kuporomoka kwa majengo nchini Kenya kumeendelea kuzua hofu kuhusu usalama wa wananchi, huku Nairobi ikiwa miongoni mwa maeneo yanayokumbwa mara kwa mara na matukio hayo yanayohusishwa na ukiukaji wa viwango vya ujenzi, usimamizi dhaifu na kushindwa kwa taasisi husika kutekeleza sheria.

Sasa muungano wa wasanifu majengo nchini umetaka hatua za haraka zichukuliwe kukomesha hali hiyo, ukisisitiza kuwa maisha ya wananchi hayawezi kuendelea kuhatarishwa kutokana na uzembe katika sekta ya ujenzi.

Katika taarifa yake, mwenyekiti wa muungano huo, Dkt. Sylvia Kasanga, amesema matukio ya hivi karibuni yanapaswa kuwa changamoto kwa taasisi zote zinazohusika na udhibiti wa ujenzi kuziba mianya iliyopo na kuwachukulia hatua wahusika wakuu.

Muungano huo sasa unamtaka Rais William Ruto kuunda kamati maalum ya kushughulikia usalama wa majengo, huku ukitaka matukio ya kuporomoka kwa majengo kutangazwa kuwa janga la kitaifa ili kuwezesha hatua za dharura katika sekta hiyo.

Wito huo unaibuka wakati historia ya Nairobi imejaa matukio ya kusikitisha ya majengo kuporomoka na kusababisha vifo na majeruhi wengi.

Miongoni mwa matukio makubwa ni kuporomoka kwa jengo la Sunbeam Supermarket kando ya Barabara ya Moi jijini Nairobi, Mei 1996, ambapo watu 16 walipoteza maisha baada ya mvua kubwa kusababisha jengo hilo kuporomoka.

Januari 2006, jengo lililokuwa eneo la Ronald Ngala pia liliporomoka na kuua watu 14, huku Desemba 2014, jengo la ghorofa tano katika eneo la Kaloleni likianguka na kusababisha vifo vya watu wanane.

Mwaka 2015, majanga mengine yalirekodiwa katika maeneo ya Huruma na Roysambu. Januari mwaka huo, jengo la makazi la ghorofa saba Huruma liliporomoka na kuua watu watano huku wengine 32 wakijeruhiwa. Aprili mwaka huohuo, jengo lililokuwa karibu na Thika Road Mall eneo la Roysambu lilianguka na kuua watu saba.

Hata hivyo, tukio lililoacha majonzi makubwa zaidi lilitokea Aprili 29, 2016, katika mtaa wa Ngei, Huruma, ambapo jengo la ghorofa sita liliporomoka kufuatia mvua kubwa, na kuua watu 51 huku wengine 140 wakijeruhiwa.

Hivi karibuni, Januari 2, 2026, jengo la ghorofa nyingi lililokuwa likijengwa katika eneo la South C liliporomoka na kuua watu wawili.

Oktoba 23, 2026, jengo la ghorofa 18 lililokuwa likijengwa Eastleigh liliporomoka na kuua watu wanane. Novemba 13, jengo la ghorofa nane Syokimau lilianguka na kuua wafanyakazi sita, huku siku iliyofuata ukuta wa eneo la ujenzi Riverside Drive ukiporomoka na kuua watu wanne.

Matukio hayo yamezidi kuibua maswali kuhusu uwajibikaji wa taasisi zinazopaswa kuhakikisha majengo yanajengwa kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa na usalama wa wananchi unalindwa.