Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) imeunda kikosi maalum cha mawakili wa serikali kitakachoshughulikia kesi za matamshi ya chuki, uchochezi na makosa yanayohusiana na uchaguzi, huku Kenya ikijiandaa kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti mwakani.
Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, Renson Igonga, amesema kikosi hicho kitakuwa na jukumu la kusimamia mashtaka dhidi ya watu watakaohusika katika makosa hayo, kufuatia kuongezeka kwa visa vya uchochezi na vurugu zinazochochewa na siasa.
Igonga amesema ofisi yake, kwa ushirikiano na wadau wengine, tayari imeanza kuwapa mafunzo maafisa watakaohusika ili kuimarisha uwezo wao wa kushughulikia na kuendesha mashtaka dhidi ya washukiwa.
Amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha wanaokiuka sheria kwa kutumia matamshi ya chuki au kuchochea ghasia wakati wa kampeni wanachukuliwa hatua za kisheria.
Hatua hiyo inajiri huku mashirika mbalimbali ya serikali na taasisi huru yakionya kuhusu kuongezeka kwa matamshi ya chuki na ubaguzi wa kikabila, hasa kwenye mitandao ya kijamii.
Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) ni miongoni mwa taasisi zilizoibua wasiwasi kuhusu mwenendo huo, ikionya kuwa unaweza kuhatarisha umoja wa kitaifa kuelekea uchaguzi ujao.
Akizungumza baada ya kuzindua ofisi mpya za ODPP mjini Naivasha, Igonga pia alitetea uamuzi wa ofisi yake kuondoa baadhi ya kesi mahakamani, akisema hatua hizo zilikuwa na sababu za msingi na zilipata idhini ya mahakama.
Amesema ODPP imekuwa ikihamasisha matumizi ya njia mbadala za kutatua migogoro nje ya mfumo wa kawaida wa mahakama ili kupunguza mrundikano wa kesi.
Kwa upande wake, Hakimu Mkuu wa Naivasha, Douglas Ogoti, amesema idara ya mahakama itashirikiana na ODPP kuimarisha upatikanaji wa haki kwa wananchi.
Ogoti amesema mahakama imejipanga kushughulikia kesi zinazohusu watoto, huku masuala hayo yakiwekewa kipaumbele katika mwezi wa huduma kwa watoto.
Jaji Cecelia Githua amesema mahakama ya Naivasha ina jumla ya kesi 1,906 za jinai ambazo hazijakamilika pamoja na zaidi ya kesi 500 za trafiki, hali inayohitaji matumizi ya njia mbadala za utatuzi wa migogoro.
Naye mwakilishi wa kikanda wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC), Ali El-Bereir, amesema Umoja wa Mataifa utaendelea kusaidia Kenya kuimarisha mfumo wa haki jinai, miundombinu na maandalizi ya uchaguzi ujao.









