Muhoozi Afunga Akaunti,Baada Ya Kumshambulia Makam Wa Rais
Jenerali Muhoozi Kainerugaba, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini Uganda, amefunga akaunti yake kuu ya mtandao wa kijamii wa X, saa chache baada ya kuchapisha jumbe zenye mashambulizi dhidi ya Makamu wa Rais wa nchi hiyo, Jessica Alupo, katika hatua iliyozua mjadala kuhusu uhusiano wa viongozi wakuu wa serikali.
Katika jumbe alizochapisha Jumatatu, Novemba 9, 2026, Muhoozi alimtuhumu Alupo kwa usaliti na kudai kuwa angeondolewa katika nafasi yake ya Makamu wa Rais hivi karibuni, bila kutoa maelezo ya kina kuhusu madai hayo.
Katika kauli nyingine, Jenerali huyo alidokeza uwezekano wa yeye mwenyewe kushika nafasi ya Makamu wa Rais, akisema kuwa kama angepewa nafasi hiyo, angeendesha serikali kwa misingi ya kijeshi ili kukabiliana na kile alichokitaja kuwa uzembe katika utendaji wa serikali.
Muhoozi pia alimshutumu Alupo kwa kumuunga mkono aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uganda, Amama Mbabazi, katika harakati zake za kuwania urais dhidi ya Rais Yoweri Museveni mwaka 2016.
Hatua ya kufunga akaunti hiyo imeibua maswali kuhusu sababu zilizomfanya Jenerali huyo kuondoka kwenye mtandao huo baada ya kuchapisha jumbe hizo, huku kukiwa hakuna maelezo rasmi yaliyotolewa kuhusu uamuzi huo.
Jessica Alupo, ambaye ni Meja Mstaafu wa Jeshi la Uganda, amekuwa Makamu wa Rais wa nchi hiyo tangu mwaka 2021, baada ya kuteuliwa na Rais Museveni.
Kwa upande wake, Muhoozi Kainerugaba ni mtoto wa Rais Yoweri Museveni, ambaye amekuwa akiongoza Uganda tangu mwaka 1986.
Jenerali Muhoozi amekuwa akivutia hisia za umma kutokana na jumbe zake za mara kwa mara kwenye mitandao ya kijamii, ambazo zimekuwa zikihusisha masuala ya kisiasa, kijeshi na uongozi wa taifa hilo.
Kufungwa kwa akaunti yake kuu ya X kunajiri huku Uganda ikiendelea kushuhudia mijadala kuhusu mustakabali wa uongozi na nafasi ya viongozi wakuu katika serikali.
Hata hivyo,kumekuwepo na cheche za maneno kutoka kwa afisa huyu wa jeshi kqenda kwa makam wa rais akihoji utendakazi wale na hali ilivyo kwa sasa.









