Serikali ya Kenya imetangaza kufungwa kabisa kwa ubalozi wake ulioko Bern, Uswisi, katika hatua inayotarajiwa kubadilisha namna Wakenya wanaoishi katika taifa hilo watakavyopata huduma za kibalozi.
Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu, Novemba 9, ubalozi wa Kenya mjini Bern uliwafahamisha raia wa Kenya na umma kwa jumla kuwa shughuli zake zitasitishwa kufuatia agizo kutoka kwa serikali ya Kenya.
Sehemu ya huduma za kibalozi (Consular Section) inatarajiwa kufungwa rasmi Jumatatu, Novemba 30, 2026, huku ubalozi huo ukielekea kusitisha shughuli zake nchini humo kabisa.
Kupitia taarifa hiyo, Wakenya ambao tayari wamejulishwa kuwa nyaraka zao zimekamilika wametakiwa kuzichukua kabla ya tarehe ya kufungwa kwa ofisi hizo.
Aidha, wale waliowasilisha maombi ya huduma za kibalozi kuanzia Novemba mosi, 2026, wameelezwa kuwa watawasiliana nao baadaye na kupewa maelekezo kuhusu namna ya kupata nyaraka zao.
Waombaji wamehitajika kuwa na kitambulisho halali pamoja na stakabadhi za maombi wanapokwenda kuchukua nyaraka hizo.
Ubalozi huo umesema maelezo kuhusu mipango mbadala ya kuwahudumia Wakenya wanaoishi nchini Uswisi yatatolewa kupitia tovuti yake na njia nyingine rasmi za mawasiliano.
Katibu Mkuu katika Wizara ya Mambo ya Nje, Korir Sing’Oei, amethibitisha hatua hiyo akisema ni sehemu ya mpango mpana wa serikali wa kurekebisha na kupanga upya uwepo wa kidiplomasia wa Kenya katika mataifa mbalimbali duniani.
Katika ujumbe wake, Sing’Oei amesema mpango huo utahusisha kufungwa kwa baadhi ya balozi na kufunguliwa kwa nyingine katika maeneo yanayoonekana kuwa na umuhimu wa kimkakati kwa maslahi ya taifa.
Ameongeza kuwa serikali itatoa taarifa ya kina kuhusu mabadiliko hayo wakati ufaao, huku akiwahakikishia Wakenya wanaoishi ughaibuni kuwa wataendelea kupata huduma za serikali licha ya mabadiliko hayo.
Ubalozi wa Kenya mjini Bern ulianzishwa rasmi Aprili 2, 2020, na umekuwa ukihudumia masuala ya kidiplomasia na mahitaji ya Wakenya nchini Uswisi.
Hata hivyo, Kenya bado ina Ujumbe wa Kudumu mjini Geneva unaoshughulikia masuala ya Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya kimataifa, ambao ni tofauti na ubalozi wa Bern.
Hatua hiyo inakuja huku serikali ikiendelea kupitia mtandao wake wa balozi za kimataifa ili kuoanisha rasilimali na vipaumbele vya sera yake.









