Rais William Ruto ametetea mageuzi yanayotekelezwa na serikali katika sekta ya kilimo, akisema yameanza kuimarisha mapato ya wakulima kupitia kupunguza gharama za pembejeo, usajili wa kidijitali wa wakulima na vita dhidi ya madalali wanaowanyonya wakulima.

Akizungumza katika soko la Kenyoro na uwanja wa Shule ya Msingi ya Nyankororo, eneo bunge la Bonchari, kaunti ya Kisii, Rais Ruto amesema wakulima wa kahawa sasa wanapata hadi shilingi 150 kwa kilo moja, kutoka wastani wa shilingi 70 waliokuwa wakilipwa awali.

Kuhusu sekta ya miwa, Rais amesema wakulima sasa wanalipwa ndani ya siku saba baada ya kuwasilisha miwa yao viwandani, huku serikali ikipanga kuanza kuwalipa bonasi. Aidha, wafanyakazi wa viwanda vya sukari sasa wanalipwa mishahara yao kila mwezi.

Katika sekta ya chai, Ruto ametangaza uwekezaji wa shilingi bilioni 4.2 kwa ajili ya kuboresha viwanda vya kuchakata chai, akisema hatua hiyo itasaidia kuongeza bei ya chai na kuhakikisha wakulima wanapata bonasi kwa usawa.

Ametaja usimamizi mbaya, viwanda vilivyochakaa na gharama kubwa za umeme kuwa miongoni mwa changamoto zinazokwamisha ukuaji wa sekta hiyo.

Aidha, Rais ameahidi kutia saini Mswada mpya wa Vyama vya Ushirika unaolenga kuimarisha usimamizi na uwajibikaji katika vyama hivyo. Mswada huo unapendekeza wakurugenzi wa vyama vya ushirika kuhudumu kwa mihula miwili pekee, kila mmoja ukiwa wa miaka mitatu.

Katika sekta ya elimu, Ruto ametetea uwekezaji wa serikali, akisema walimu 100,000 wameajiriwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, huku wengine 20,000 wakitarajiwa kuajiriwa mwezi Desemba.

Ameongeza kuwa serikali imejenga madarasa 23,000 ya ziada ili kuboresha mazingira ya kujifunzia shuleni.

Rais alikuwa akizungumza baada ya kuzindua ujenzi wa barabara ya kilomita 22 ya Kenyoro SDA–Riana Market–Kerina, ambayo amesema itarahisisha usafirishaji wa bidhaa na kukuza biashara katika eneo la Bonchari.

Rais pia alizindua rasmi Shule ya Msingi ya Nyankororo, ambako madarasa 12 yamejengwa kwa msaada wa kampuni ya Safaricom.

Kwa upande wake, Gavana wa Kisii Simba Arati aliibua wasiwasi kuhusu tofauti katika malipo ya bonasi kwa wakulima wa chai, akitaka wakulima kutoka eneo la Magharibi mwa Kenya kupewa uwakilishi wa haki katika usimamizi wa viwanda vya chai.

Makatibu wa Baraza la Mawaziri Opiyo Wandayi na Julius Ogamba, wabunge pamoja na viongozi wengine wa kaunti walihudhuria hafla hiyo.