Matumizi ya teknolojia ya Akili Unde (AI) na mifumo ya kiotomatiki isiyodhibitiwa yanaweza kuhatarisha ajira za mamilioni ya watu duniani, huku kukiwa na wito wa kuweka maadili ya kibinadamu mbele katika maendeleo ya kiteknolojia.

Kiongozi wa Kanisa Katoliki, Papa Leo XIV, ametoa onyo kuhusu athari zinazoweza kusababishwa na kuongezeka kwa matumizi ya Akili Unde na mifumo ya mashine kufanya kazi ambazo hapo awali zilikuwa zikitekelezwa na binadamu.

Katika ujumbe wake, Papa amesema kuwa licha ya teknolojia kuwa na nafasi muhimu katika maendeleo ya jamii, matumizi yake yasiyozingatia maadili yanaweza kuhatarisha ajira na kudhoofisha maendeleo jumuishi ya binadamu.

Amesisitiza kuwa teknolojia inapaswa kuongozwa na misingi ya maadili, akionya kuwa mifumo ya kompyuta na algoriti haiwezi kuchukua nafasi ya uwezo wa binadamu kufanya maamuzi yenye busara wala thamani ya mfanyakazi katika jamii.

Papa ameeleza kuwa maendeleo ya kiteknolojia yanapaswa kuwanufaisha watu wote badala ya kuacha sehemu kubwa ya jamii katika hali ya ukosefu wa ajira na fursa za kujikimu kimaisha.

Amesema upatikanaji wa ajira kwa kila mtu unapaswa kupewa kipaumbele katika sera za umma na mifumo ya kiuchumi, akitaja ajira kuwa mojawapo ya vigezo muhimu vya kupima ubora wa kibinadamu katika mfumo wowote wa maendeleo.

Kwa mujibu wa Papa, maendeleo hayawezi kuchukuliwa kuwa kamili iwapo yanakuza teknolojia na uzalishaji huku yakipuuza mahitaji, haki na utu wa wafanyakazi.

Onyo hilo linajiri wakati matumizi ya Akili Unde yakizidi kupanuka katika sekta mbalimbali zikiwemo mawasiliano, elimu, viwanda, biashara na huduma za kifedha, huku baadhi ya mifumo ya kiotomatiki ikichukua majukumu yaliyokuwa yakifanywa na wafanyakazi.

Mjadala kuhusu athari za teknolojia hiyo kwa soko la ajira umeendelea kushika kasi duniani, huku kukiwa na maswali kuhusu namna ya kuhakikisha maendeleo ya kiteknolojia hayaongezi pengo la kiuchumi kati ya watu.

Papa ametoa ujumbe huo kupitia mtandao wa kijamii wa X wakati wa safari yake ya kitume nchini Argentina, akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha kuwa teknolojia inabaki kuwa chombo cha kumhudumia binadamu na si kumwondolea nafasi yake katika jamii.

Amehimiza serikali na wadau wa uchumi kuhakikisha kuwa sera na maamuzi yao yanazingatia utu wa binadamu, haki za wafanyakazi na upatikanaji wa fursa za ajira kwa wote.