Wakenya 1,392 Wapata Fidia, Ukiukaji Haki Za Kibinadamu
Jopo la Fidia kwa Waathiriwa wa Ukiukaji wa Haki za Kibinadamu nchini Kenya limeshughulikia jumla ya madai 1,392, huku waathiriwa 236 waliopoteza maisha wakifidiwa pamoja na mamia ya wengine waliopata majeraha na hasara za kiuchumi.
Mwenyekiti wa jopo hilo, Makau Mutua, amesema waathiriwa zaidi ya 700 waliojeruhiwa wamepokea fidia, huku wengine 140 wakilipwa kutokana na hasara za kiuchumi zilizotokana na ukiukaji wa haki zao.
Aidha, waathiriwa 16 wa ukatili wa kingono pia wamefidiwa, hatua ambayo amesema inaonyesha juhudi za serikali katika kushughulikia madhara yaliyowapata wananchi kutokana na ukiukaji wa haki za kibinadamu.
Mutua amesema serikali ina wajibu mkubwa wa kuhakikisha kila mwananchi anakuwa salama na anaishi maisha yenye maana, akisisitiza umuhimu wa kuwajibisha wale wanaohusika na madhara dhidi ya raia, wakiwemo maafisa wa serikali.
Amesema hakuna taifa lisilo na visa vya ukiukaji wa haki za kibinadamu, hata katika demokrasia zilizoendelea, lakini kinachotofautisha mataifa ni hatua zinazochukuliwa baada ya ukiukaji huo kuripotiwa.
Mwenyekiti huyo pia amepuuzilia mbali madai kwamba ni mtu mmoja pekee aliyefidiwa, akisema jopo hilo limefanya kazi na waathiriwa wengi na familia zao.
Amesema jopo limewatembelea baadhi ya familia zilizokubali kupokea wajumbe wake nyumbani, huku likiendelea kushughulikia madai yaliyowasilishwa.
Mutua ameeleza kuwa jopo hilo limekuwa likipokea na kuchunguza madai mbalimbali ili kuhakikisha wanaostahili wanapata fidia kulingana na madhara waliyopata. Aina za madhara yanayoshughulikiwa ni pamoja na vifo, majeraha ya kimwili, ukatili wa kingono na upotevu wa mali au kipato.
Hata hivyo, amesema taarifa za baadhi ya waathiriwa zitachapishwa baada ya kufanyiwa marekebisho ili kulinda utambulisho wa wale ambao hawataki majina yao kuwekwa wazi.
Amesema jopo hilo pia limekuwa likishirikiana na familia za waathiriwa walio tayari kushiriki katika mchakato huo, akisisitiza kuwa ulinzi wa faragha ni muhimu katika kuhakikisha haki zao zinaheshimiwa.
Jopo hilo limeahidi kutoa taarifa zaidi kuhusu kazi yake, huku tarehe Novemba 14 ikiwa ndiyo muda uliowekwa wa kukamilisha shughuli zake.









