Gavana wa Kaunti ya Elgeyo Marakwet, Wisley Rotich, anakabiliwa na ukosoaji mkali kufuatia makabiliano ya hadharani na naibu wake, Profesa Grace Cheserek, katika hafla ya uwezeshaji iliyofanyika eneo la Kapyego, Kaunti Ndogo ya Marakwet Mashariki.

Makabiliano hayo yaliyoshuhudiwa Jumapili, Novemba 8, yalizua mjadala baada ya gavana huyo kumkatiza naibu wake alipokuwa akilihutubia umati, akimtaka kushuka jukwaani na kumshutumu kwa tabia ya kitoto.

Hata hivyo, Cheserek alikaidi agizo hilo akisisitiza kuwa alikuwa na haki ya kumaliza hotuba yake bila kukatizwa.

Katika video zilizosambaa mitandaoni, naibu gavana huyo alisikika akimwambia Rotich kuwa hakuwa amemwalika kwenye hafla hiyo na kwamba angeendelea kuzungumza na kueleza yote aliyokuwa nayo moyoni.

Mzozo huo ulizidi kupamba moto baada ya Cheserek kuanza kuikosoa serikali ya kaunti akidai kuwa imeshindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo, hususan katika sekta za afya na elimu.

Pia aliituhumu serikali ya Rotich kwa kujikita katika kugawa misaada ya fedha na bidhaa kwa wananchi ili kupata uungwaji mkono badala ya kutafuta suluhu za kudumu kwa changamoto zinazowakabili wakazi.

Hali ilizidi kuwa tete kuelekea mwisho wa hotuba yake, huku gavana akiripotiwa kuwaagiza walinzi wake kumwondoa naibu wake jukwaani. Video za tukio hilo zilionyesha afisa mmoja wa usalama akiingilia kati na kumsindikiza Cheserek kutoka eneo hilo.

Makabiliano hayo yamekosolewa na viongozi mbalimbali wa wanawake katika eneo la North Rift, ambao wamesema kitendo hicho kinadhalilisha wanawake waliochaguliwa kushikilia nyadhifa za uongozi.

Viongozi hao wamemtaka Rotich kumwomba Cheserek msamaha rasmi, wakisisitiza kuwa tofauti za kisiasa hazipaswi kutumiwa kama sababu ya kuwanyima viongozi wanawake heshima wanayostahili.

Hii si mara ya kwanza kwa wawili hao kuzozana hadharani.

Mnamo Agosti mwaka huu, walikwaruzana wakati wa uzinduzi wa Biblia iliyotafsiriwa kwa lugha ya Marakwet katika eneo la Tot baada ya Rotich kuwatambulisha maafisa wengine bila kumtaja naibu wake.

Mvutano huo pia umeongezeka baada ya Cheserek kutangaza kuwa hatakuwa mgombea mwenza wa Rotich katika uchaguzi mkuu wa 2027.

Sasa wakazi wanahoji mustakabali wa ushirikiano kati ya viongozi hao wawili, ambao walichaguliwa kwa tiketi moja mwaka 2022.