Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) inataka kifungo cha miaka 30 jela alichopewa mwanamume aliyepatikana na hatia ya kumbaka mpwawe mwenye umri wa miaka 10 kiongezwe hadi kifungo cha maisha.
Mwendesha mashtaka Sidi Kirenge aliwasilisha ombi hilo mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu ya Eldoret, Antony Ndung'u, akisema adhabu iliyotolewa na mahakama ya chini kwa Cleophas Kipsang haikuzingatia kikamilifu uzito wa kosa alilotenda.
Kirenge alieleza kuwa umri mdogo wa mwathiriwa, uhusiano wa kifamilia kati yake na mshtakiwa pamoja na madhara yaliyotokana na unyanyasaji huo vilipaswa kuzingatiwa wakati wa kutoa hukumu.
Mahakama pia iliambiwa kuwa Kipsang alimwambukiza mtoto huyo virusi vya Ukimwi (VVU) wakati wa unyanyasaji wa kingono, jambo ambalo upande wa mashtaka unasema limeongeza madhara ya kimwili na kisaikolojia aliyokumbana nayo mwathiriwa.
ODPP ililaumu mahakama ya chini kwa kuipa uzito mkubwa hali ya kiafya ya mshtakiwa wakati wa kutoa hukumu, ikisisitiza kuwa mazingira ya kosa hilo yalihitaji adhabu kali zaidi.
Kipsang alihukumiwa kifungo cha miaka 30 gerezani Aprili 27, 2026, baada ya kupatikana na hatia ya kufanya ngono na jamaa wa karibu, kosa linalojulikana kama incest.
Sasa upande wa mashtaka unaitaka Mahakama Kuu kupitia upya mwenendo na rekodi za kesi hiyo na kuongeza adhabu hiyo kwa mujibu wa Kifungu cha 20 cha Sheria ya Makosa ya Kingono, kinachotaja kifungo cha maisha kwa makosa yanayohusisha ubakaji wa mtoto aliye chini ya umri wa miaka 18.
Jaji Ndung'u anatarajiwa kutoa maelekezo kuhusu ombi hilo mwezi ujao.
Katika tukio jingine, Mahakama ya Hola, kaunti ya Tana River, imewahukumu wanaume wawili kifungo cha maisha baada ya kupatikana na hatia ya kuwabaka watoto katika visa viwili tofauti.
Katika kesi ya kwanza, mwanamume mwenye umri wa miaka 65 alihukumiwa kifungo cha maisha baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 11.
Mahakama ilielezwa kuwa tukio hilo lilitekelezwa katika tarehe tofauti mwezi Oktoba mwaka jana katika kijiji cha Kone.
Mshtakiwa alipatikana na hatia ya ubakaji chini ya Kifungu cha 8(1) na 8(2) cha Sheria ya Makosa ya Kingono ya mwaka 2006.
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Hola, Edward Too, alisema upande wa mashtaka uliwasilisha ushahidi wa kutosha kuthibitisha kosa hilo, akibainisha kuwa maelezo ya mtoto yaliungwa mkono na ushahidi wa mashahidi wengine pamoja na rekodi za matibabu.
Too alisema adhabu hiyo inaakisi uzito wa kosa na inalenga kuzuia vitendo kama hivyo dhidi ya watoto.
Katika kesi ya pili, Bakari Dhadho Salim alipatikana na hatia ya kumbaka mtoto wa miaka 12 kati ya Juni 18 na 26 mwaka huu katika kijiji cha Mikinduni.
Mahakama hiyo pia ilimhukumu kifungo cha maisha, ikiashiria msimamo wa mahakama kuhusu makosa ya kingono yanayowalenga watoto.









