Takriban watu 11 wamefariki dunia na wengine karibu 50 kujeruhiwa baada ya ajali mbili kubwa za barabarani kuhusisha takriban magari 50 katika barabara kuu ya Trakia nchini Bulgaria.

Ajali hizo zilitokea Jumanne, Novemba 10, katika eneo la kusini mashariki mwa Bulgaria, karibu na mji wa Yambol, huku ukungu mzito ukitajwa kuwa chanzo kikuu cha mikasa hiyo iliyosababisha msururu wa magari kugongana.

Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Ndani nchini humo, hali ya hewa ilikuwa mbaya kiasi cha kupunguza pakubwa mwonekano kwa madereva, na kusababisha magari kushindwa kusimama kwa wakati baada ya ajali za awali kutokea.

Ajali ya kwanza ilitokea katika kilomita ya 289 kwenye barabara inayoelekea mji wa Burgas, huku nyingine ikitokea kilomita ya 294, karibu na makutano ya Zimnitsa, kwenye barabara inayoelekea mji mkuu wa Sofia.

Magari yaliyohusika katika ajali hizo ni pamoja na magari madogo na malori, huku baadhi yakipinduka, kuharibika vibaya na mengine kuishia nje ya barabara kutokana na nguvu za migongano hiyo.

Timu za polisi, wazima moto na wahudumu wa ambulensi zilitumwa katika maeneo hayo kuendesha shughuli za uokoaji na kuwasaidia manusura waliokuwa wamenasa ndani ya mabaki ya magari yaliyosambaratika.

Takriban watu 50 waliripotiwa kujeruhiwa na kupelekwa katika hospitali za maeneo ya Sliven, Yambol na Burgas kwa matibabu, huku kukiwa na hofu kwamba huenda idadi hiyo ikaongezeka kutokana na uwezekano wa watu wengine kuwa bado wamenasa kwenye magari yaliyoharibika.

Mkaguzi Mkuu wa Polisi katika Kurugenzi ya Mkoa ya Yambol, Todor Mishinev, alisema kipaumbele cha kwanza kwa maafisa wa usalama ni kukamilisha shughuli za uokoaji kabla ya kuanza uchunguzi rasmi kubaini mazingira yaliyochangia ajali hizo.

Kutokana na mkasa huo, Waziri Mkuu wa Bulgaria, Rumen Radev, amesitisha shughuli zake zilizokuwa zimepangwa kufanyika katika mji wa Varna.

Serikali pia ilighairi mkutano wa Baraza la Mawaziri uliokuwa umepangwa kufanyika Jumanne, huku ndege ya serikali ikitumwa mjini Burgas kusaidia kuwasafirisha majeruhi waliokuwa wakihitaji matibabu maalumu katika hospitali za Sofia.

Aidha, ndege za kijeshi aina ya Spartan ziliandaliwa kusaidia shughuli za usafirishaji wa majeruhi kwenda hospitalini.

Hadi sasa, mamlaka hazikuwa zimetangaza rasmi utambulisho wa waliofariki, huku Rais wa Bunge la Ulaya, Roberta Metsola, akituma salamu za rambirambi kwa familia zilizopoteza wapendwa wao na kuwapongeza wahudumu wa dharura kwa juhudi zao za uokoaji.