Takriban wanajeshi 66 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) wamehukumiwa adhabu ya kifo kwa makosa ya woga vitani, uasi na kukataa kutii maagizo ya wakuu wao wa kijeshi.

Hukumu hiyo ilitolewa na mahakama ya kijeshi mjini Walikale, katika jimbo la Kivu Kaskazini mashariki mwa nchi hiyo, kufuatia kesi iliyowahusisha jumla ya wanajeshi 71 waliokuwa wakikabiliwa na tuhuma mbalimbali za utovu wa nidhamu wakati wa operesheni za kupambana na waasi.

Wanajeshi wanne waliachiliwa huru baada ya mahakama kutowapata na hatia, huku mwingine akihukumiwa kifungo cha miaka 10 gerezani.

Kwa mujibu wa jeshi la DRC, kesi hiyo inalenga kurejesha nidhamu na uwajibikaji miongoni mwa wanajeshi wanaopambana na makundi yenye silaha katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo ambalo limekumbwa na miongo kadhaa ya machafuko.

Ripoti zinaeleza kuwa wanajeshi hao walikamatwa Oktoba 20 mjini Walikale, wakituhumiwa kuacha vituo vyao vya kazi na kukimbia wakati wa mapigano dhidi ya wapiganaji wa muungano wa waasi wa Front for the Refoundation of the Nation (FRN), unaojumuisha kundi la M23.

Jeshi la Congo limekuwa likikabiliwa na changamoto za muda mrefu za utovu wa nidhamu, ukosefu wa uratibu na mpangilio dhaifu katika operesheni zake za kijeshi, hali inayodaiwa kudhoofisha juhudi za serikali kukabiliana na makundi ya waasi.

Wanajeshi pia wamekuwa wakilalamikia mishahara duni na ukosefu wa vifaa vya kutosha, huku jeshi likikabiliwa na shutuma za kushindwa kudumisha weledi miongoni mwa wanajeshi wake.

Mwezi uliopita, wanajeshi wengine 27 walihukumiwa kifo kwa makosa yanayofanana baada ya kudaiwa kujiondoa katika mstari wa mbele wakati wa mapigano dhidi ya waasi.

Mwaka 2024, serikali ya DRC iliondoa marufuku ya utekelezaji wa adhabu ya kifo iliyokuwa imedumu kwa takriban miaka 20, ikisema hatua hiyo ililenga kukabiliana na wasaliti ndani ya jeshi pamoja na watu wanaohusika na uasi, ugaidi na uhalifu wa kivita.

Uamuzi huo ulikosolewa vikali na mashirika ya kutetea haki za binadamu yaliyotahadharisha kuhusu uwezekano wa ukiukaji wa haki za washtakiwa na matumizi mabaya ya adhabu hiyo.

Hata hivyo, hakuna hukumu rasmi ya kifo iliyotekelezwa tangu marufuku hiyo iondolewe.

Takwimu zilizokusanywa na shirika la utangazaji la Ufaransa RFI zinaonyesha kuwa tangu mwanzoni mwa mwaka 2025, angalau wanajeshi 507 wamehukumiwa, wakiwemo 381 waliopewa adhabu ya kifo.

Aidha, Oktoba 2025, aliyekuwa Rais wa DRC Joseph Kabila alihukumiwa kifo akiwa hayupo mahakamani kwa makosa yaliyohusisha uhaini na uhalifu wa kivita. Kabila alikanusha tuhuma hizo na hakuhudhuria kesi yake kujitetea. Baadaye alitajwa kuwa kiongozi wa muungano wa waasi wa FRN.