Walimu 9,830 wanaofundisha katika shule za Junior Secondary nchini Kenya wamekuwa kiini cha mvutano kati ya vyama vya KNUT na KUPPET, huku kila chama kikidai kuwa ndicho kinachopaswa kuwawakilisha katika masuala ya ajira na maslahi yao.
Mzozo huo unahusu chama kinachopaswa kupokea michango ya kila mwezi kutoka kwa walimu hao, ambao wengi wao walikuwa wanachama wa KNUT kabla ya kuhamishiwa kufundisha katika shule za Junior Secondary.
Baadhi ya walimu wameibua malalamishi baada ya kugundua kuwa michango iliyokuwa ikikatwa kutoka kwenye mishahara yao na kuelekezwa KNUT ilikuwa imehamishiwa KUPPET bila wao kuwasilisha maombi ya kubadilisha chama.
Mwalimu Doreen Kiremi kutoka Meru Central, ambaye anasema amekuwa mwanachama wa KNUT tangu mwaka 2015, ni miongoni mwa walioathiriwa na mabadiliko hayo.
Mwalimu mwingine, Regina Omondi kutoka Nairobi, pia anasema hakuwahi kuomba kujiunga na KUPPET licha ya michango yake kuanza kuelekezwa kwa chama hicho.
Hata hivyo, Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) imesema ilitekeleza mabadiliko hayo kufuatia agizo la Mahakama lililotolewa Septemba 17, 2026.
Mkurugenzi wa masuala ya sheria, ajira na mahusiano ya wafanyakazi TSC, Cavin Anyuor, amesema tume ilichukua hatua hiyo kwa kuzingatia agizo la mahakama, huku ikitambua walimu wa Junior Secondary kama walimu wa sekondari.
Lakini katika mabadiliko ya hivi karibuni ya kisheria, Mahakama ya Ajira na Mahusiano Kazini ilitengua agizo hilo Oktoba 29 na kutupilia mbali kesi iliyowasilishwa na KUPPET.
Anyuor amesema kutokana na uamuzi huo, TSC haitapeleka tena michango ya walimu hao kwa KUPPET kuanzia mishahara ya mwezi Novemba.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa KUPPET, Akelo Misori, anasisitiza kuwa walimu wa Junior Secondary wanapaswa kuwa wanachama wa chama hicho kwa kuwa wanafanya kazi katika mfumo wa elimu ya sekondari.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa KNUT, Collins Oyuu, anapinga msimamo huo akisema walimu wanapaswa kuwa na uhuru wa kuchagua chama kitakachowawakilisha.
Oyuu amerejelea makubaliano ya mwaka 2018 kati ya vyama hivyo yaliyoweka utaratibu wa uwakilishi kwa kuzingatia taasisi ambako mwalimu anahudumu, huku KNUT ikiwakilisha walimu wa shule za msingi na KUPPET wale wa sekondari.
Mzozo huo unaangazia changamoto za uwakilishi wa walimu kufuatia mageuzi ya mfumo wa elimu nchini, ambapo baadhi ya walimu walioajiriwa katika shule za msingi wamehamishiwa kufundisha katika shule za Junior Secondary.









