Naibu Gavana wa kaunti ya Migori Joseph Mahiri ametoa wito wa kudumisha amani katika maeneo ya Kuria Magharibi na Kuria Mashariki kufuatia kisa cha wizi wa mifugo kilichosababisha vifo vya watu wawili.

Mahiri amewataka wakazi wa maeneo hayo kujiepusha na vitendo vya kulipiza kisasi, akisisitiza kuwa migogoro inayotokana na wizi wa mifugo inapaswa kutatuliwa kwa njia za kisheria badala ya kutumia nguvu.

Naibu gavana huyo amesema ni muhimu jamii kushirikiana na vyombo vya usalama ili kuhakikisha waliohusika katika mauaji hayo wanakamatwa na kufikishwa mbele ya sheria.

Wito wake unajiri huku kukiwa na wasiwasi kuhusu uwezekano wa kuzuka kwa uhasama baina ya jamii zinazoishi katika maeneo hayo kufuatia vifo hivyo.

Kwa upande wake,Moses Burure Maarufu kama Musa, mfanyabiashara wa dhahabu eneo la Kehancha, amesisitiza kuwa hakuna sababu inayopaswa kuhalalisha kupoteza maisha ya binadamu, akiwataka wakazi kuweka kando tofauti zao na kudumisha mshikamano.

Musa amesema viongozi wa eneo hilo wana jukumu la kuhakikisha hali ya utulivu inarejea, huku wakazi wakihimizwa kutafuta suluhu kupitia mazungumzo na mifumo iliyowekwa kisheria.

Aidha, amewataka wazee wa jamii, machifu na viongozi wengine kushirikiana katika juhudi za kuzuia migogoro inayoweza kuchochewa na visa vya wizi wa mifugo.

Kwa upande mwingine,Peter Rioba,ambaye ni kiongozi wa dini anasema jamii ya wakuria ni moja ambayo inatakiwa kumgeukiwa Mungu na kuepuka visa ambavyo matokeo yake ni laana.

Anasema,wapo wanaotamani kadhia hiyo kuendelea ili wapate nafasi ya kupora mali ya watu na wapo wanaokesha wakiomba amani kupatikana.

Awali Musa Burure,aliiitaka serikali kuongeza doria na operesheni za kiusalama katika maeneo yanayokumbwa na visa vya wizi wa mifugo, huku wakazi wakihimizwa kutoa taarifa kuhusu watu wanaoshukiwa kujihusisha na uhalifu huo.

Wakazi pia wametakiwa kuepuka kujichukulia sheria mkononi kwa kuwa hatua hiyo inaweza kusababisha vifo zaidi na kuvuruga amani katika jamii.

Wizi wa mifugo umekuwa mojawapo ya changamoto za kiusalama katika baadhi ya maeneo ya Kuria, huku viongozi wakitaja ushirikiano wa jamii na vyombo vya usalama kuwa muhimu katika kukabiliana na tatizo hilo.

Mathlan, umuhimu wa kulinda maisha ya wananchi na kudumisha amani ili shughuli za kiuchumi na kijamii ziendelee bila hofu ya mashambulizi ni jambo la kheri.