Uchaguzi Wa 2027: Murkomen Atoa Uhakikisho Kwa Jumuiya Ya Kimataifa
Waziri wa Usalama wa kitaifa, Kipchumba Murkomen, amewahakikishia washirika wa kimataifa kuwa Kenya inaendelea kujiandaa kuhakikisha uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 unafanyika kwa amani na utulivu.
Murkomen amesema kuwa Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) inaendelea kuimarisha mikakati ya kiusalama ili kuhakikisha usalama unadumishwa katika hatua zote za uchaguzi, kuanzia kampeni, upigaji kura, kuhesabu kura hadi kutangazwa kwa matokeo.
Akizungumza Jumatatu, Novemba 9, wakati wa mkutano na wakuu wa ujumbe wa kundi la wafadhili wa wakimbizi (RDG) pamoja na washirika wengine wa kimataifa jijini Nairobi, Murkomen amesema serikali imeweka maandalizi ya kutosha kukabiliana na changamoto zozote za kiusalama zinazoweza kujitokeza wakati wa uchaguzi.
Waziri huyo amekiri kuwa kumekuwa na matukio ya hapa na pale wakati wa kampeni za kisiasa, lakini akasema baadhi yake yamekuwa yakikuza zaidi ya ukubwa wake halisi, huku akisisitiza kuwa hali hiyo inadhibitika.
Ameeleza kuwa serikali ina imani kuwa kipindi chote cha uchaguzi, ikiwemo baada ya kutangazwa kwa matokeo, kitapita kwa amani.
Mbali na masuala ya uchaguzi, mkutano huo pia ulijadili maendeleo ya utekelezaji wa mpango wa Shirika (Shirika Plan), ambao ni mpango wa serikali wa miaka 12 unaolenga kubadilisha kambi za wakimbizi kuwa miji jumuishi inayoweza kujitegemea kiuchumi na kijamii.
Murkomen ameishukuru jumuiya ya kimataifa kupitia kundi la wafadhili wa wakimbizi kwa kuendelea kushirikiana na Kenya katika kutekeleza mpango huo.
Amesema hatua kubwa zimepigwa katika maeneo ya ulinzi wa kijamii, ujumuishaji wa kifedha, upatikanaji wa bima ya afya pamoja na kuanzishwa kwa mifumo ya uongozi wa serikali za manispaa katika maeneo yanayohifadhi wakimbizi.
Katika hatua nyingine, Murkomen amesema wakimbizi waliosajiliwa na wenye vitambulisho rasmi vya wakimbizi sasa wanaweza kutumia huduma za M-Pesa.
Amesema hatua hiyo ni muhimu katika kuwawezesha wakimbizi kupata huduma za kifedha na kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali nchini Kenya.
Haya yanajiri huku jamii ya kimataifa ikitilia shaka uchaguzi mkuu ujao kutokana na hali ya ushindani iliopo kwa sasa









