Mauti Ya Kijana Wa Maiaka 17 AirBnB:Washukiwa Wawili Mikononi Mwa Polisi

Familia ya kijana mwenye umri wa miaka 17, Michael Kimani, inataka haki kutendeka kufuatia kifo chake cha kutatanisha, kinachochunguzwa na polisi baada ya kudaiwa kusukumwa kutoka ghorofa ya tisa ya jengo la Airbnb eneo la Gwakairu.

Familia hiyo iliyotumbukia katika majonzi makubwa inasema imepoteza watu wawili wa karibu katika kipindi cha siku nne pekee, baada ya mama yake Michael kufariki dunia siku nne kabla ya kifo cha mwanawe.

Wakiwa wameongozwa na Mary Watiri, jamaa hao wamewataka maafisa wa polisi kuharakisha uchunguzi wa kifo hicho na kuhakikisha waliohusika wanachukuliwa hatua za kisheria.

Walisema wanapitia kipindi kigumu cha maombolezo, huku wakihangaika kupata majibu kuhusu mazingira yaliyopelekea kifo cha kijana huyo, ambaye alikuwa na umri mdogo na maisha yake yakiwa bado mbele yake.

Polisi tayari wamewakamata wanaume wawili wanaodaiwa kuwa katika chumba hicho cha Airbnb pamoja na Michael wakati wa tukio hilo, huku mshukiwa wa kike akiripotiwa kutoroka na bado akitafutwa na maafisa wa usalama.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, Michael aliondoka nyumbani Jumatano usiku wa wiki iliyopita kwenda kumtembelea rafiki yake wa kiume, ambaye pia alikuwa akiomboleza kifo cha mamake.

Hata hivyo, haijabainika ni kwa nini vijana hao waliishia katika nyumba ya Airbnb, wala kilichotokea ndani ya chumba hicho kabla ya Michael kuanguka kutoka ghorofa ya tisa.

Familia yake sasa inataka polisi kufichua ukweli kuhusu mazingira ya kifo chake, ikiwemo kubaini iwapo kulikuwa na ugomvi au tukio jingine lililosababisha kijana huyo kuanguka kutoka jengo hilo.

Wakati huo huo, kukamatwa kwa washukiwa wawili kunatarajiwa kusaidia uchunguzi wa polisi, huku juhudi zikiendelea kumtafuta mshukiwa wa kike anayehusishwa na tukio hilo.

Familia ya Michael imeendelea kusisitiza kuwa inataka haki, ikiwataka polisi kuhakikisha uchunguzi unakamilishwa bila kuchelewa na wahusika wote wanafikishwa mbele ya sheria iwapo ushahidi utathibitisha kuhusika kwao.

Kifo hicho kimezua maswali kuhusu mazingira ya usalama wa vijana na matukio yanayotokea katika nyumba zinazokodishwa kwa muda mfupi kupitia mifumo ya Airbnb.