Kenya imeimarisha ushirikiano wake na Shirika la Afya Duniani (WHO) katika kukabiliana na ugonjwa wa Ebola, huku nchi hiyo ikifikisha siku 21 bila kuripoti kisa kipya cha maambukizi ya virusi vya Bundibugyo Ebola.
Waziri wa Afya Aden Duale amekutana na ujumbe wa WHO ukiongozwa na Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika, Profesa Yakub Janabi, kujadili hatua zilizopigwa katika kudhibiti mlipuko huo pamoja na mikakati ya kuimarisha usalama wa afya nchini.
Mkutano huo umeangazia mafanikio yaliyopatikana katika ufuatiliaji wa maambukizi, upimaji wa sampuli, matibabu ya wagonjwa na maandalizi ya kukabiliana na dharura za kiafya.
Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni, Kenya imethibitisha jumla ya visa tisa vya Ebola, ambavyo vyote vinahusishwa na mlolongo mmoja wa maambukizi. Wagonjwa sita wamepona na kuruhusiwa kutoka hospitalini, wawili wamefariki dunia huku mmoja akiendelea kupatiwa matibabu.
Hakuna ushahidi wa maambukizi kusambaa katika jamii, huku kisa cha mwisho kikithibitishwa Oktoba 19, 2026.
Katika mazungumzo hayo, Duale aliishukuru WHO kwa msaada wa kitaalamu na vifaa vya kukabiliana na ugonjwa huo, ikiwemo mifumo 12 ya kisasa ya kupima virusi kwa kutumia teknolojia ya PCR pamoja na kituo cha matibabu ya Ebola chenye vitanda 28.
Aidha, zaidi ya wasafiri 760,000 wamekaguliwa katika vituo vya kuingia nchini, huku sampuli 736 zikipimwa katika maabara tano maalumu na zaidi ya wahudumu 7,300 wa afya wakipatiwa mafunzo ya kukabiliana na ugonjwa huo.
Waziri huyo amesisitiza umuhimu wa kuendeleza ufuatiliaji wa karibu, uchunguzi wa haraka wa visa vinavyoshukiwa na ukaguzi wa wasafiri katika mipaka ili kuzuia uwezekano wa maambukizi mapya.
Hata hivyo, Kenya bado haijaanza rasmi kipindi cha siku 42 kinachohitajika kabla ya kutangaza kumalizika kwa mlipuko huo. Kipindi hicho kitaanza baada ya mgonjwa wa mwisho kupona na kuruhusiwa kutoka kituo cha matibabu.
Duale pia ameelezea wasiwasi kuhusu baadhi ya nchi kuweka vizuizi vya safari na masharti ya visa kwa wasafiri kutoka Kenya, akitaka WHO kusaidia kuhakikisha hatua za afya ya umma zinaongozwa na ushahidi wa kisayansi na kanuni za kimataifa za afya.
Wakati huo huo, pande hizo zimekubaliana kuandaa mpango wa pamoja wa kuimarisha uwezo wa Kenya kukabiliana na milipuko ya magonjwa, ikiwemo mafunzo ya wataalamu, vifaa vya uchunguzi na uimarishaji wa mifumo ya afya.
WHO imeendelea kusisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kudumisha tahadhari kutokana na kuendelea kwa maambukizi ya Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).









