Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema hana muda wa kufuatilia kiwango halisi cha utajiri wake akisisitiza kuwa tayari anamiliki fedha nyingi, hata kabla ya kuingia madarakani, huku akifichua kuwa mwanawe ndiye anayesimamia masuala yake ya kifedha.

Trump alitoa kauli hiyo katika mahojiano maalumu na kipindi cha 60 Minutes cha kituo cha televisheni cha CBS, alipoulizwa kuhusu ripoti ya jarida la Forbes iliyodai kuwa utajiri wake umeongezeka kwa takribani dola bilioni tatu za Marekani.

Akijibu swali hilo, Trump alisema hajishughulishi na kufuatilia thamani ya mali zake wala kuzungumzia masuala ya fedha na mwanawe anayesimamia utajiri wake. Alisema hana wasiwasi kuhusu ongezeko au upungufu wa mali zake kwa kuwa tayari ana fedha nyingi, huku akikiri kuwa huenda utajiri wake umeongezeka lakini hana takwimu kamili.

Aliongeza kuwa hali yake ya kifedha ilikuwa nzuri hata kabla ya kuingia Ikulu ya White House, akisisitiza kuwa hategemei mshahara wa urais na kwamba hachukui malipo hayo.

Kauli hizo zimeibua mjadala kuhusu utajiri wake na namna anavyosimamia masuala ya kifedha akiwa madarakani, hasa ikizingatiwa kuwa shughuli zake za kibiashara zimekuwa zikifuatiliwa kwa karibu tangu aliporejea Ikulu ya White House.

Katika mahojiano hayo, Trump pia alizungumzia matokeo ya uchaguzi wa katikati ya muhula (Midterm Elections), ambapo chama chake cha Republican kilipata pigo baada ya kupoteza udhibiti wa Baraza la Wawakilishi na Seneti.

Akijibu kuhusu kushindwa kwa chama chake, Trump alijitetea akisema yeye mwenyewe hakuwa mgombea katika uchaguzi huo, licha ya kufanya kampeni kwa nguvu kuwaunga mkono wagombea wa Republican.

Alidai kuwa wapiga kura hawakuwapendelea baadhi ya wagombea wa chama chake na kwamba haikuwa rahisi kuhamishia wagombea hao umaarufu aliokuwa nao yeye.

Trump pia alikiri kuwa vita dhidi ya Iran, kupanda kwa bei ya mafuta na hisia hasi za baadhi ya Wamarekani kuhusu Israel zilichangia kushindwa kwa chama chake.

Hata hivyo, alitetea rekodi yake ya kiuchumi akisema Marekani inaendelea kufanya vizuri, huku akilaumu ujumbe wa kisiasa wa chama chake kwa kushindwa kuwaeleza wananchi mafanikio ya serikali.

Matokeo hayo yamezua mjadala ndani ya Republican kuhusu uongozi wa Trump na athari za sera zake kwa mustakabali wa chama hicho, huku shinikizo likiongezeka kwa utawala wake kuelekea kipindi kingine cha kisiasa.