Mwigizaji Russel Brand Ahukumiwa Miaka 10,Ubakaji Na Unyanyasaji Wa Kingono
Mwigizaji na mchekeshaji maarufu wa Uingereza, Russell Brand, amehukumiwa kifungo cha miaka 10 na miezi sita gerezani baada ya kupatikana na hatia ya ubakaji na makosa matatu ya unyanyasaji wa kingono dhidi ya wanawake wanne.
Hukumu hiyo imetolewa Jumatatu katika Mahakama ya Southwark Crown Court jijini London, baada ya kesi iliyodumu kwa takribani wiki nne na kufichua tuhuma za vitendo vya kingono vilivyotekelezwa kati ya mwaka 2004 na 2009.
Brand, mwenye umri wa miaka 51, alipatikana na hatia ya kumbaka mwanamke mmoja aliyekuwa shabiki wake nyumbani kwake mwaka 2009, pamoja na kuwanyanyasa kingono wanawake wengine watatu katika matukio tofauti.
Mahakama ilisikiliza ushahidi kwamba baadhi ya vitendo hivyo vilitokea katika maeneo ya burudani, kituo cha redio na studio ya kurekodia matangazo jijini London.
Jaji Joel Bennathan alitoa hukumu hiyo baada ya kuzingatia uzito wa makosa hayo, madhara ya kisaikolojia waliyopata waathiriwa pamoja na mazingira ambayo makosa hayo yalitekelezwa.
Upande wa mashtaka ulikuwa umeitaka mahakama kutoa adhabu kali, ukisema Brand alitumia umaarufu na ushawishi wake katika tasnia ya burudani kuwanyanyasa wanawake na kujihisi kuwa anaweza kutenda makosa bila kuwajibishwa.
Wakati wa kusikilizwa kwa hukumu, baadhi ya waathiriwa walielezea namna matukio hayo yalivyoathiri maisha yao, yakiwemo kupoteza kujiamini, kupata msongo wa mawazo na kuendelea kukumbwa na kumbukumbu za matukio hayo.
Hata hivyo, Brand aliachiliwa huru dhidi ya mashtaka mawili ya ubakaji na shtaka moja la kujaribu kufanya unyanyasaji wa kingono.
Mwigizaji huyo alikuwa amekana mashtaka yote yaliyokuwa yakimkabili, akisisitiza kuwa mahusiano yake ya kingono yalikuwa ya makubaliano kati ya wahusika.
Brand alizuiliwa rumande baada ya kupatikana na hatia wiki iliyopita, mahakama ikikataa ombi la kumwachilia kwa dhamana akisubiri hukumu.
Polisi wa Metropolitan London wamesema uchunguzi kuhusu madai mengine ya ubakaji yanayomhusisha Brand unaendelea, huku kesi hiyo ikiibua mjadala kuhusu matumizi mabaya ya umaarufu na mamlaka katika tasnia ya burudani.
Je,kesi hiyo ya Russel haiwezi kupata apili?









