Umoja wa Mataifa (UN) umeeleza kuwa kuzuiliwa kwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, ni kinyume cha sheria za kimataifa.
Aidha UN inasema Serikali ya Tanzania inapaswa kumuachilia huru mara moja.
Katika uamuzi wake, Kikundi Kazi cha Umoja wa Mataifa kuhusu Kuzuiliwa Kiholela (UN Working Group on Arbitrary Detention) kilihitimisha kuwa kuzuiliwa kwa Lissu kunakiuka haki zake za msingi, ikiwemo uhuru wa kujieleza, kushiriki katika shughuli za kisiasa na kupata haki ya kusikilizwa kwa mujibu wa sheria.
Kikundi hicho kilitoa maoni yake Februari 23, 2026, kikisema hatua dhidi ya kiongozi huyo wa upinzani inakiuka masharti kadhaa ya Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu na Mkataba wa Kimataifa kuhusu Haki za Kiraia na Kisiasa.
Mbali na kutaka aachiliwe mara moja, Umoja wa Mataifa umeitaka serikali kuhakikisha Lissu anapata fidia na hatua nyingine za kurekebisha madhara aliyoyapata kutokana na kuzuiliwa kwake.
Lissu alikamatwa Aprili 9, 2025, baada ya kuhudhuria mkutano wa kisiasa mjini Mbinga, mkoani Ruvuma, ambako alikuwa akihamasisha msimamo wa Chadema wa kutaka mageuzi ya uchaguzi kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka huo.
Baadaye alishtakiwa kwa uhaini, kosa ambalo linaweza kuadhibiwa kwa kifo chini ya sheria za Tanzania.
Katika tathmini yake, kikundi hicho cha Umoja wa Mataifa kilieleza wasiwasi kuhusu msingi wa kisheria wa kuzuiliwa kwa Lissu, pamoja na madai ya ukiukaji wa haki yake ya kupata kesi ya haki.
Pia kilikosoa matumizi ya shtaka lisiloruhusu dhamana bila tathmini maalumu ya umuhimu wa kuendelea kumzuilia mshtakiwa, kikisema hatua hiyo haiendani na viwango vya kimataifa vya haki za binadamu.
Uamuzi huo unaongeza shinikizo la kimataifa kwa Serikali ya Tanzania kuhusu namna inavyoshughulikia kesi ya Lissu, ambaye amekuwa mmoja wa wakosoaji wakuu wa serikali na mtetezi wa mageuzi ya kisiasa nchini humo.
Hata hivyo, serikali ya Tanzania imepinga madai kwamba kuzuiliwa kwa Lissu ni kiholela, ikisisitiza kuwa kesi yake inaendelea mahakamani na kwamba hatua zilizochukuliwa dhidi yake zina msingi wa sheria za nchi.
Katika mawasilisho yake mbele ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, serikali ilisema Lissu anapata fursa ya kujitetea na kwamba suala hilo linapaswa kuachwa lishughulikiwe na mahakama.
Kwa sasa, uamuzi wa kikundi hicho cha Umoja wa Mataifa unaendeleza mjadala kuhusu haki za kisiasa, uhuru wa kujieleza na mwenendo wa kesi zinazowakabili viongozi wa upinzani nchini Tanzania.









