Wakati visa vya unyakuzi wa ardhi na udanganyifu katika umiliki wa mali vikiendelea kuzua wasiwasi nchini, Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) imeelekeza kidole cha lawama kwa mapungufu ya kiutendaji na ukiukaji wa maadili katika sekta ya upimaji ardhi, ikiwataka wataalamu husika kuimarisha uadilifu na uwajibikaji.

Mwenyekiti wa EACC, Askofu Dk. David Oginde, amesema wataalamu wa upimaji ardhi wana jukumu muhimu katika kulinda rasilimali za wananchi, akionya kuwa kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia weledi kunaweza kuchochea vitendo vya ufisadi na migogoro ya umiliki wa ardhi.

Akizungumza mjini Naivasha wakati wa Kongamano la 11 la Kikanda la Afrika la Taasisi ya Masoroveya, Oginde alielezea wasiwasi wake kuhusu visa vya unyakuzi wa ardhi pamoja na matumizi ya nyaraka bandia zinazohusiana na umiliki wa ardhi.

Alisema kuwepo kwa mianya katika mifumo ya uthibitishaji na usimamizi wa taarifa za ardhi kunatoa nafasi kwa watu wasio waaminifu kujipatia mali kwa njia zisizo halali, hali inayohitaji hatua madhubuti kutoka kwa wataalamu na taasisi zinazohusika.

Oginde aliwataka masoroveya kuzingatia viwango vya juu vya kitaaluma na maadili katika shughuli zao, akisisitiza kuwa taaluma hiyo inapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha taarifa za ardhi zinakuwa sahihi, za kuaminika na zinazoweza kuthibitishwa.

Aidha, alionya kuwa kutoshughulikia mapungufu yaliyopo katika sekta hiyo kunaweza kusababisha madhara makubwa zaidi kwa wananchi na kudhoofisha juhudi za serikali katika kulinda haki za umiliki wa ardhi.

Kongamano hilo lililoandaliwa mjini Naivasha limewakutanisha viongozi na wadau kutoka sekta mbalimbali za Afrika kujadili mikakati ya kukuza uwekezaji endelevu na mchango wa wataalamu wa upimaji ardhi katika maendeleo ya kiuchumi.

Kaulimbiu ya mwaka huu ililenga kuchochea uwekezaji endelevu kupitia mchango wa masoroveya katika uchumi wa baharini, uchumi unaozingatia mazingira na uchumi wa ujenzi.

Kwa upande wao, Rais wa Taasisi ya Masoroveya, Eric Nyadimo, pamoja na naibu wake Nelly Mbugua, walielezea dhamira yao ya kuimarisha uadilifu, weledi na uwajibikaji miongoni mwa wanachama wa taasisi hiyo.

Viongozi hao pia walieleza utayari wao wa kushirikiana na EACC kutafuta suluhu kwa changamoto zinazoikabili sekta hiyo, huku wakisisitiza umuhimu wa kuimarisha viwango vya kitaaluma ili kusaidia kukuza uwekezaji endelevu barani Afrika.