Kampuni ya habari ya Standard Group PLC imemteua Dkt. Naim Bilal Yaseen kuwa Afisa Mkuu Mtendaji (CEO) mpya, akitarajiwa kuanza rasmi majukumu yake Novemba 1, 2026, kuchukua nafasi ya Chaacha Mwita anayeondoka katika wadhifa huo.

Uteuzi huo unafuatia mchakato wa ushindani wa kuwasaka viongozi wapya uliofanywa na bodi ya kampuni hiyo, huku Yaseen akitarajiwa kuongoza taasisi hiyo katika kipindi ambacho sekta ya habari inakabiliwa na mabadiliko makubwa ya kiteknolojia na kidijitali.

Yaseen ana tajriba ya zaidi ya miaka 30 katika tasnia ya habari, taasisi za umma na usimamizi wa mashirika, akiwa amewahi kushikilia nyadhifa mbalimbali za uongozi katika taasisi muhimu nchini Kenya.

Kabla ya uteuzi huo, aliwahi kuhudumu kama Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji la Kenya (KBC) kuanzia Machi 2019 hadi mwaka 2022.

Pia aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Masuala ya Umma na Mawasiliano katika Idara ya Mahakama (Judiciary), nafasi aliyohudumu kati ya mwaka 2012 na 2017.

Katika safari yake ya kikazi, Yaseen pia amewahi kufanya kazi katika Shirika la Nation Media Group kama msimamizi wa habari katika kituo cha televisheni cha NTV, kati ya mwaka 1999 na 2007.

Aidha, aliwahi kushikilia wadhifa wa Naibu Mkurugenzi na Mkuu wa Mawasiliano ya Umma serikalini, kabla ya kuhamia katika Idara ya Mahakama.

Kitaaluma, Yaseen ana Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Masomo ya Mawasiliano kutoka Chuo Kikuu cha Moi. Pia ana Shahada ya Uzamili katika Sera za Mawasiliano kutoka City, University of London, pamoja na Shahada ya Uzamili ya Usimamizi wa Biashara (MBA).

Vilevile, ana shahada ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Afrika Kusini (UNISA) na ni wakili wa Mahakama Kuu ya Kenya.

Bodi ya Standard Group imesema inatarajia Yaseen kuimarisha utendaji wa kibiashara wa kampuni hiyo, kuongeza uwekezaji katika majukwaa ya kidijitali na kulinda uhuru wa uhariri unaochangia kuimarisha imani ya umma katika habari.

Standard Group ni mojawapo ya mashirika kongwe ya habari nchini Kenya, likimiliki magazeti ya The Standard na The Nairobian, vituo vya televisheni vya KTN na KTN News pamoja na Radio Maisha na Spice FM.

Mwita, ambaye alichukua nafasi ya Marion Gathoga-Mwangi kwa kaimu kuanzia Julai 2025, alithibitishwa kuwa Mkurugenzi Mkuu rasmi Aprili 1, 2026.