Wizara ya Afya nchini imetangaza hatua mpya katika juhudi za kudhibiti mlipuko wa ugonjwa wa Ebola baada ya wagonjwa wawili kati ya saba waliokuwa wakitengwa hospitalini kupatikana hawana virusi hivyo katika vipimo vya awali.
Mkurugenzi Mkuu wa Afya nchini, Dk. Patrick Amoth, amesema wagonjwa hao wawili watapimwa tena baada ya saa 72 ili kuthibitisha matokeo hayo, huku wengine watano wakiendelea kuwa katika hali thabiti chini ya uangalizi wa madaktari.
Tangazo hilo linajiri huku nchi ikirekodi siku tatu mfululizo bila kuripoti kisa kipya cha maambukizi, hatua inayotajwa kuwa ishara ya mafanikio katika juhudi za kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo hatari.
Kenya imethibitisha jumla ya visa tisa vya Ebola katika mlipuko huu, huku watu wawili wakifariki dunia, hali inayoweka kiwango cha vifo katika asilimia 22.2.
Visa vyote tisa vinahusishwa na mtu mmoja wa kwanza kuambukizwa, raia wa Kenya aliyesafiri kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kupitia Uganda kabla ya kufariki dunia Oktoba 5.
Watu wengine wanane waliambukizwa kufuatia kisa hicho cha kwanza, wakiwemo wanafamilia wanne na wahudumu wanne wa afya waliomhudumia mgonjwa huyo kabla ya kubainika kuwa alikuwa na Ebola.
Miongoni mwa waliofariki ni jamaa wa familia hiyo mwenye umri wa miaka 65, aliyefariki Oktoba 23.
Dkt. Amoth amesema uchunguzi haujabaini mnyororo wowote wa maambukizi nje ya watu waliokuwa tayari wametambuliwa na kufuatiliwa, akisisitiza kuwa hakuna ushahidi wa ugonjwa huo kuenea katika jamii.
Wizara ya Afya pia imethibitisha kufuatilia watu wote 135 waliokuwa wamekutana na wagonjwa, wakiwemo tisa waliokuwa nje ya Kenya. Nchi walizokuwa wamekimbilia ziliarifiwa kupitia kanuni za kimataifa za kudhibiti dharura za kiafya.
Kati ya watu hao, 20 walikamilisha kipindi cha siku 21 cha ufuatiliaji Oktoba 26 na kuruhusiwa kurejea nyumbani baada ya kutokuwa na dalili za maambukizi.
Watu wengine 98 wanaendelea kuwekwa karantini, huku waliosalia wakitarajiwa kuachiliwa kwa awamu kuanzia Novemba 3 baada ya kukamilisha muda wa ufuatiliaji.
Dkt. Amoth amesema mamlaka za afya zinaendelea kufuatilia hali ya wagonjwa na watu waliokuwa kwenye hatari ya kuambukizwa ili kuzuia uwezekano wa mlipuko huo kuongezeka.
Hata hivyo, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuchukua tahadhari hadi pale hatari ya maambukizi itakapodhibitiwa kikamilifu.









