Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna ametangaza rasmi kuanza kwa safari mpya ya kisiasa kupitia vuguvugu la Linda Mwananchi, akiwashutumu washirika wa serikali ya Rais William Ruto kwa kujaribu kuzuia juhudi zao za kuanzisha chama kipya cha kisiasa.
Sifuna amesema safari ya kuunda chama hicho imekuwa ngumu, licha ya Katiba ya Kenya kumpa kila mwananchi haki ya kuunda chama cha kisiasa na kujihusisha na shughuli za kisiasa.
Akizungumza wakati wa kutangaza viongozi wa muda wa chama hicho, Sifuna aliwashukuru kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kwa kuruhusu mikutano ya kisiasa kufanyika katika ngome zao bila washiriki kushambuliwa.
Hata hivyo, alidai baadhi ya mikutano yao ilivurugwa na watu aliowahusisha na mrengo wa Broad-Based Government.
Sifuna pia alidai serikali imeweka vikwazo katika juhudi zao za kuanzisha chama hicho, akisema hawakutarajia upinzani huo ungeimarisha azma yao ya kuendelea na siasa.
Alijitambulisha kama mwanafunzi wa kisiasa wa marehemu Raila Odinga, akisema uzoefu wake ndani ya ODM utawasaidia kujenga chama chenye miundo thabiti kote nchini.
Katika kauli iliyolenga kuonyesha ukubwa wa mgawanyiko ndani ya ODM, Sifuna alisema wanaondoka na sehemu kubwa ya miundo ya chama hicho, akitumia maneno ya kejeli kudai kuwa ODM imebakia na “mende na kunguni.”
Aidha, alidai kuwa baada ya kutangaza chama cha Equitable Party, Rais Ruto alianza kutumia ujumbe unaofanana na kaulimbiu yao ya usawa, akimtuhumu kwa kunakili mawazo ya wengine.
Sifuna amesema chama hicho kinakusudia kufungua ofisi katika kaunti zote 47, huku kikitarajia kufanya Kongamano la Kitaifa la Wajumbe (NDC) tarehe 13 mwezi ujao ili kuweka rasmi miundo ya uongozi.
Miongoni mwa viongozi wa muda waliotangazwa ni Sifuna kama kiongozi wa chama, Caroli Omondi kama katibu mkuu, Godfrey Osotsi kama mwenyekiti na Pauline Njoroge kama naibu katibu mkuu.
Richard Onyonka ameteuliwa kuwa mweka hazina wa kitaifa, huku George Natembeya akipewa jukumu la kuongoza kampeni za urais.
Sifuna pia aliomba msamaha kwa Gachagua na Kalonzo, akisema baadhi ya wafuasi wao wameamua kujiunga na vuguvugu hilo.
Kwa upande wake, Osotsi alisema ODM imebadilika tangu kifo cha Raila Odinga, akidai chama hicho kimekuwa karibu mno na serikali.
Vuguvugu hilo linasisitiza kuwa linaunga mkono umoja wa upinzani, likisema hiyo ndio njia ya kushindana na Rais Ruto katika uchaguzi ujao wa 2027.









