Mwanamume Wa Miaka 24 Auawa Kwa Kudungwa Kisu Nyali
Polisi jijini Mombasa wanachunguza mauaji ya mwanamume mwenye umri wa miaka 24 yaliyotokea katika makazi ya Vescon One Apartments, eneo la Kadzandani, kaunti ya Mombasa.
Ian Mwendwa Muriithi anadaiwa kuuawa kwa kudungwa kisu kifuani wakati wa ugomvi uliotokea kati yake na mpenzi wake, katika hali ambayo sasa imewaacha maafisa wa upelelezi wakichunguza chanzo cha mzozo huo.
Kwa mujibu wa ripoti ya polisi, tukio hilo liliripotiwa majira ya saa tisa alfajiri baada ya walinzi wa makazi hayo kufahamishwa kuhusu ugomvi uliokuwa ukiendelea ndani ya mojawapo ya nyumba katika jengo hilo.
Walipofika katika eneo la tukio, walinzi hao walimkuta Muriithi akiwa amelala bila fahamu karibu na mlango wa bafu, huku akiwa na jeraha la kudungwa kisu upande wa kushoto wa kifua.
Hata hivyo, juhudi za kumsaidia hazikufua dafu, kwani alithibitishwa kufariki dunia katika eneo la tukio.
Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa marehemu alikuwa amehusika katika mabishano na mpenzi wake, Joan Murugi, mwenye umri wa miaka 23, muda mfupi kabla ya kupatikana akiwa amejeruhiwa.
Katika hatua nyingine, Murugi pamoja na mshukiwa mwingine wamekamatwa na polisi kuhusiana na mauaji hayo huku uchunguzi ukiendelea kubaini nafasi ya kila mmoja katika tukio hilo.
Maafisa wa upelelezi pia wamechukua kisu kimoja cha jikoni kinachoshukiwa kutumika katika kutekeleza mauaji hayo kama sehemu ya ushahidi utakaosaidia uchunguzi.
Mwili wa Muriithi umehamishiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali Kuu ya Pwani, ambako unasubiri kufanyiwa uchunguzi wa maiti ili kubaini chanzo kamili cha kifo chake.
Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) imeanzisha uchunguzi wa kina kuhusu mazingira yaliyopelekea kifo hicho, huku polisi wakitarajiwa kukusanya ushahidi zaidi na kurekodi taarifa kutoka kwa watu wanaoweza kusaidia kufichua kilichotokea ndani ya nyumba hiyo.
Maafisa wa polisi hawajafichua zaidi kuhusu sababu ya ugomvi huo wala uhusiano wa mshukiwa wa pili na marehemu.
Hata hivyo,familia ya marehemu inasubiri kuona haki ikitendeka na wahuskia kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria









