Wataalamu wa Umoja wa Mataifa (UN) wameishutumu Serikali ya Somalia kwa kuingilia uhuru wa mahakama baada ya kumwondoa Jaji Mkuu Bashe Yusuf Ahmed na kumwapisha mrithi wake bila kufuata taratibu za kikatiba.

Wataalamu hao wa haki za binadamu wamesema hatua hiyo ni ukiukaji wa wazi wa uhuru wa mahakama na utawala wa sheria, wakitaka Ahmed arejeshwe madarakani pamoja na kurejeshwa kwa ulinzi wa majaji walioathiriwa na uamuzi huo.

Katika taarifa iliyotolewa Geneva, Novemba 12, 2026, wataalamu hao walilaani uamuzi wa Serikali kumwondoa Ahmed kupitia amri ya Rais Novemba 4, bila idhini ya Bunge au pendekezo kutoka Tume ya Huduma za Mahakama.

Aidha, walieleza kuwa Serikali ilimwapisha Ibrahim Idle Suleiman kuwa Jaji Mkuu mpya Novemba 7, siku tatu tu baada ya kuondolewa kwa Ahmed, bila kufuata taratibu zinazotakiwa kisheria.

Mvutano huo ulitokea wakati Mahakama ya Juu ilipokuwa ikijiandaa kutoa uamuzi kuhusu uhalali wa hatua za hivi karibuni za kuongeza muda wa mihula ya Rais na Bunge kutoka miaka minne hadi mitano.

Novemba 5, majaji watano wa Mahakama ya Juu waliendelea kusikiliza kesi hiyo na kuamua kuwa nyongeza ya mihula hiyo ilikuwa kinyume cha sheria, wakisema muda wa Rais na Bunge ulikuwa umeisha na kuagiza uchaguzi ufanyike ndani ya siku 90.

Katika uamuzi huo, majaji pia walitangaza kuondolewa kwa Ahmed kuwa kinyume cha Katiba, wakisema hatua hiyo ililenga kuzuia Mahakama kushughulikia suala la kuongeza mihula ya Rais na Bunge.

Hata hivyo, Serikali ilikataa kutekeleza maagizo hayo, huku ikipeleka mamia ya maafisa wa usalama katika Mahakama ya Juu hatua ambayo wataalamu wa UN walisema ililenga kuvuruga shughuli za mahakama na kuwatisha majaji.

Wataalamu hao pia walifichua kuwa majaji saba wa Mahakama ya Juu walinyimwa ulinzi wao binafsi licha ya kuwepo kwa vitisho vya kiusalama, huku wakizuiwa kusafiri.

“Tunalaani vitisho na juhudi za kuwatisha majaji. Ulinzi wao binafsi unapaswa kurejeshwa mara moja,” walisema wataalamu hao, huku wakitaka vikosi vya usalama kuondoka katika Mahakama ya Juu.

Walisema uhuru wa mahakama ni nguzo muhimu ya demokrasia na utawala wa sheria, huku wakisisitiza kuwa majaji wanapaswa kufanya maamuzi bila shinikizo, vitisho au kuingiliwa na mamlaka nyingine.

Wataalamu hao walionya kuwa kuingilia uhuru wa mahakama kunaweza kudhoofisha juhudi za Somalia za kukabiliana na ugaidi na kuimarisha usalama, wakati nchi hiyo ikiendelea kukabiliwa na tishio la kundi la Al-Shabaab.

Wakisisitiza msimamo wao, wataalamu hao walitaka Ahmed kurejeshwa katika nafasi yake kisheria na kuhakikisha usalama wa majaji wote nchini Somalia.