Vyama vya wafanyakazi katika vyuo vikuu vya umma nchini, vikiwemo Chama cha Wahadhiri wa Vyuo Vikuu (UASU), Chama cha Wafanyakazi wa Vyuo Vikuu (KUSU) na KUDHEIHA, vimetangaza kuanza rasmi kwa mgomo wao kuanzia usiku wa leo.

Akizungumza wakati wa kutangaza kuanza kwa mgomo huo, Katibu wa Kuratibu Mipango wa UASU, Jacob Musembi, alisema vyama hivyo vimekataa pendekezo la nyongeza ya mishahara ya asilimia nne kwa mwaka lililotolewa na Baraza la Kitaifa la Vyuo Vikuu vya Umma (IPUCCF).

Musembi alisema pendekezo hilo linakinzana na makubaliano yaliyofikiwa katika mazungumzo ya awali kati ya vyama vya wafanyakazi na waajiri.

Aliongeza kuwa pendekezo kuhusu bima ya afya kwa wafanyakazi wa vyuo vikuu pia halijakidhi matarajio yao, akisema kiwango kilichopendekezwa ni cha chini ikilinganishwa na bima inayotolewa kwa wafanyakazi wengine katika sekta ya umma.

Kwa mujibu wa Musembi, utekelezaji wa Mkataba wa Makubaliano ya Pamoja wa 2025–2029 (CBA) pia umechelewa, licha ya makubaliano ya awali yaliyowekwa kuhusu utekelezaji wake.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa KUSU, Dkt. Charles Mukhwaya, aliishutumu Serikali kupitia Wizara ya Elimu kwa kushindwa kutekeleza ahadi na makubaliano iliyofikia na wafanyakazi wa vyuo vikuu.

Dkt. Mukhwaya alisema kuanzia kesho shughuli za masomo zinatarajiwa kuathirika katika vyuo vikuu vyote vya umma nchini kutokana na mgomo huo.

Aliwataka wahadhiri na wafanyakazi wengine wa vyuo vikuu kushiriki kikamilifu katika mgomo huo, akiwataka kufika katika Chuo Kikuu cha Nairobi kesho, ambapo hatua hiyo itazinduliwa rasmi.

Mgomo huo unatarajiwa kuathiri shughuli za ufundishaji, mitihani na huduma nyingine za vyuo vikuu vya umma endapo hakutakuwa na makubaliano kati ya vyama vya wafanyakazi na Serikali.