Chama cha Wanasheria nchini (LSK) kimeandaa maandamano kulaani kutoweka kwa wakili Abshir Ahmedsadak Abdi, ambaye familia yake inasema alitekwa na watu waliokuwa wamejihami kwa bunduki katika mazingira ambayo bado hayaijaeleweka.
Wanasheria hao wameitaka serikali kueleza aliko Abshir na kuhakikisha anarudishwa salama, wakionya kuwa vitisho na utekaji wa mawakili vinahatarisha utawala wa sheria pamoja na uhuru wa kutekeleza majukumu yao ya kisheria.
Katika maandamano hayo, Rais wa Jumuiya ya Wanasheria wa Afrika Mashariki (EALS), Ramadhan Abubakar, alisema mawakili wameanza kukabiliwa na vitisho na unyanyasaji, akionya kuwa hali hiyo inaweza kuenea na kuwakumba pia wanahabari na makundi mengine katika jamii.
Abubakar alisema mawakili hawawezi kutekeleza wajibu wao ipasavyo iwapo serikali itashindwa kuhakikisha usalama wao.
Alisisitiza kuwa shambulio dhidi ya wakili ni shambulio dhidi ya utawala wa sheria, akisema wanasheria wamesimama kutetea Katiba na wanataka kuachiwa kwa mwenzao.
Kwa upande wake, Rais wa LSK, Charles Kanjama, alisema kuwa iwapo kuna tuhuma zozote dhidi ya Abshir, anapaswa kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka badala ya kutoweshwa.
Alisisitiza kuwa hakuna mtu anayepaswa kujichukulia sheria mkononi na kutaka wakili huyo aachiwe mara moja.
Kanjama alitangaza kuwa msafara wa waandamanaji utaelekea katika makao makuu ya polisi, Jogoo House, ambako watawasilisha memoranda kwa Inspekta Jenerali wa Polisi, Douglas Kanja, wakitaka hatua zichukuliwe kubaini aliko Abshir.
Ndugu wa wakili huyo, Zakaria Abshir, alisema familia imekuwa bila taarifa za aliko ndugu yao kwa siku sita, akisisitiza kuwa hawaoni tukio hilo kama kutoweka kwa kawaida bali utekaji nyara.
Alisema familia ina wazazi ambao hawajui aliko mwanao na akaomba serikali itimize wajibu wake wa kulinda raia.
Aidha, alikosoa kile alichokitaja kuwa ni juhudi za kuchafua jina la Abshir badala ya kuweka wazi aliko.
Zakaria alisema watu wanaotuhumiwa kwa makosa makubwa wamewahi kufikishwa mahakamani, hivyo Abshir anapaswa kupewa nafasi sawa ya kujibu tuhuma zozote mbele ya sheria.
Maandamano hayo yanafanyika huku kukiwa na maswali kuhusu watu wawili waliokuwa na Abshir na ambao pia wameripotiwa kutoweka.
Familia ya Ayub Mohamud Maalim imeripoti kutopatikana kwake katika Kituo cha Polisi cha Kilimani.
Kesi ya habeas corpus inayotaka mamlaka zimfikishe Abshir mahakamani na kueleza aliko inaendelea, huku mahakama ikitarajiwa kutoa uamuzi kuhusu ombi hilo Jumanne ijayo.
Polisi na vyombo vya uchunguzi vimeeleza kuwa vinafanya uchunguzi, huku wakili huyo akiendelea kutopatikana.









