Macho na masikio ya Watanzania na wananchi kote duniani leo yanaelekezwa jijini Dar es Salaam, ambako Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, inatarajiwa kutoa hukumu katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Antipas Lissu.

Hukumu hiyo inayosubiriwa kwa hamu na wasiwasi na wafuasi wa chama hicho pamoja na wadau wa siasa nchini Tanzania, inatarajiwa kusomwa kuanzia saa tatu asubuhi mbele ya jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, akisaidiwa na Jaji James Karayemaha na Jaji Ferdinand Kiwonde.

Katika ujumbe wake kuelekea siku hii muhimu, Lissu amesema yuko tayari kukabiliana na matokeo yoyote yatakayotokana na uamuzi wa mahakama, akisisitiza kuwa maisha lazima yaendelee bila kujali hukumu itakavyokuwa.

Kiongozi huyo wa upinzani ameeleza kuwa iwapo atapata fursa ya kutoka gerezani, hatua yake ya kwanza itakuwa kuelekea Arusha, ambako anakusudia kushiriki katika mazishi ya kaka yake aliyefariki hivi karibuni.

Lissu amekuwa akiumizwa na kutoweza kushiriki kikamilifu katika kipindi cha mwisho cha maisha ya kaka yake pamoja na maandalizi ya mazishi kutokana na kuwekwa mahabusu kwa muda mrefu.

Katika ujumbe wake, amesisitiza kuwa hukumu yoyote haitakuwa mwisho wa safari yake ya kisiasa wala mapambano yake ya kudai haki na demokrasia nchini Tanzania.

Lissu pia amewahimiza Watanzania kujitokeza kwa wingi kushuhudia hukumu hiyo, akitambua kuwa siku hii ni muhimu katika safari yake ya kisiasa na maisha yake binafsi.

Wito huo unaambatana na msimamo wa Chadema kuwataka wanachama, wafuasi, viongozi wa kisiasa na watetezi wa haki za binadamu kufika mahakamani kufuatilia mwenendo wa utoaji wa hukumu.

Kwa upande mwingine, Jeshi la Polisi limewahakikishia wananchi kuwa linaendelea kusimamia usalama jijini Dar es Salaam, likisisitiza kuwa litahakikisha amani na utulivu vinadumishwa wakati wa shughuli za mahakama.

Polisi wameeleza kuwa wanatambua haki ya wananchi kufika mahakamani kufuatilia mashauri, lakini wameonya dhidi ya mipango yoyote ya vurugu, fujo au vitendo vya uhalifu.

Lissu alikamatwa Aprili 9, 2025, wilayani Mbinga, mkoani Ruvuma, alipokuwa akihamasisha wananchi kudai mageuzi ya sheria na mfumo wa uchaguzi.

Siku iliyofuata, Aprili 10, 2025, alifunguliwa rasmi kesi ya uhaini jijini Dar es Salaam.

Mashtaka yanahusishwa na kauli anazodaiwa kutoa Aprili 3, 2025, kuhusu kuzuia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Upande wa mashtaka umedai kuwa kauli hizo zilikuwa na nia ya kuitishia Serikali, madai ambayo Lissu ameyapinga katika utetezi wake.

Hukumu ya leo inatarajiwa kuwa hatua muhimu katika kesi iliyodumu kwa zaidi ya mwaka mmoja, huku ikifuatiliwa kwa karibu ndani na nje ya Tanzania.

Kwa Lissu, hata hivyo, ujumbe wake umebaki kuwa mmoja: maisha lazima yaendelee, na lolote litakalotokea halitakuwa mwisho wa maisha.