Hali ya sintofahamu imezidi kutanda kuhusu kutoweka kwa wakili wa Nairobi Abshir Ahmedsadak Abdi, baada ya kubainika kuwa watu wengine wawili waliokuwa na uhusiano wa karibu naye pia wameripotiwa kutoweka katika mazingira ambayo bado hayajafahamika.
Miongoni mwa watu hao ni Ayub Muhammad Malim, mkazi wa Mombasa ambaye alikuwa amesafiri hadi Nairobi kutembelea familia yake kabla ya kutoweka akiwa safarini pamoja na wakili Abshir.
Familia ya Ayub imeeleza kuwa imekuwa ikimtafuta tangu Novemba Mosi, 2026, bila mafanikio, hali iliyowalazimu kufika katika Kituo cha Polisi cha Kilimani Alhamisi, Novemba 5, kuwasilisha taarifa rasmi na kuomba msaada wa vyombo vya usalama kubaini aliko.
Ndugu wa Ayub wamesema wamekuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu usalama wake, wakieleza kuwa ni mtu muhimu katika familia yake ambaye ana watoto, mke na ndugu wanaomtegemea.
Familia hiyo imeitaka serikali na vyombo vya usalama kuingilia kati na kusaidia kufuatilia nyendo zake ili kuhakikisha anapatikana akiwa salama.
Aidha, utambulisho wa mtu wa pili aliyeripotiwa kutoweka haukuwekwa wazi na familia iliyozungumza na wanahabari kuhusu tukio hilo.
Hata hivyo, mwanaharakati wa haki za binadamu Hussein Khalid kutoka shirika la Vocal Africa ameibua hofu kwamba Ayub huenda alichukuliwa pamoja na wakili Abshir katika tukio linalohusishwa na kutoweka kwa wakili huyo.
Khalid amesema kuna mashaka kwamba Ayub huenda alitekwa nyara pamoja na Abshir, huku akitaka uchunguzi wa kina kufanyika ili kubaini kilichowapata.
Kutoweka kwa watu hao kunajiri siku chache baada ya familia ya Abshir kuwasilisha ombi katika Mahakama Kuu ya Milimani, Nairobi, ikitaka vyombo vya usalama kueleza aliko wakili huyo na kuhakikisha anafikishwa mahakamani akiwa hai au amefariki.
Abshir aliripotiwa kutoweka Novemba Mosi, 2026, baada ya kudaiwa kutekwa na watu wenye silaha katika Barabara ya Muchai, karibu na barabara ya Ngong jijini Nairobi. Gari lake aina ya Toyota Premio lilipatikana likiwa limetelekezwa katika eneo hilo.
Mahakama imehusika katika juhudi za kutafuta majibu kuhusu kutoweka kwake, huku familia, wanasheria na wanaharakati wakitaka vyombo vya usalama kuwajibika.
Kwa sasa, hakuna taarifa rasmi iliyothibitisha walipo Abshir, Ayub na mtu huyo mwingine, huku mazingira ya kutoweka kwao yakiendelea kuibua maswali mengi.









