Aliyekuwa Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua, ametangaza kifo cha dada yake mkubwa, Eunice Nyangari Gachagua, aliyefariki dunia jana mjini Naro Moru, Kaunti ya Nyeri, akiwa na umri wa miaka 77.
Katika ujumbe wa rambirambi aliouchapisha, Gachagua amesema familia ya marehemu Mzee Nahashon Gachagua Reriani na Martha Kirigo Gachagua imeingia katika majonzi kufuatia kifo cha Eunice, ambaye alikuwa mzaliwa wa kwanza katika familia yao.
Gachagua amemtaja marehemu kama nguzo muhimu ya familia, akisema alikuwa amechukua nafasi ya mama tangu kifo cha mama yao miaka saba iliyopita.
Amesema Eunice alikuwa amekuwa akitoa mwongozo, ushauri na faraja kwa wanafamilia, akijitwika jukumu la kuhakikisha familia inaendelea kuwa na mshikamano baada ya kufiwa na mama yao.
Katika salamu zake za rambirambi, Gachagua ameeleza masikitiko yake huku akituma pole kwa watoto wa marehemu, Waithera na Murimi, wajukuu, vitukuu pamoja na familia nzima ya Reriani.
Amesema yeye na familia yake wanashiriki kikamilifu katika maumivu yanayowakabili ndugu na jamaa kufuatia msiba huo, akisisitiza kuwa pengo lililoachwa na marehemu litakuwa gumu kuzibika.
Gachagua pia amemshukuru Mungu kwa kumpa Eunice miaka 77 ya maisha duniani, akisema familia itamkumbuka kwa hekima yake, upendo, uchangamfu na nyakati nzuri walizoshiriki pamoja.
Kwa mujibu wa Gachagua, marehemu alikuwa mtu mwenye furaha na moyo wa upendo ambaye uwepo wake uliwapa wanafamilia faraja na furaha.
Amesema ushauri wake wa busara, ukarimu na namna alivyokuwa akiwajali wengine ni miongoni mwa mambo ambayo familia itayakosa sana kufuatia kifo chake.
Kifo cha Eunice kinakuja miaka saba baada ya familia hiyo kumpoteza mama yao, kipindi ambacho marehemu alijitokeza na kuwa sura ya malezi na uongozi kwa ndugu zake.
Gachagua amehitimisha ujumbe wake kwa kumuombea marehemu pumziko la amani, huku akitoa sala kwamba nuru ya milele imwangazie daima.
Familia, ndugu na marafiki sasa wanaomboleza kuondokewa na mwanamke ambaye alikuwa na nafasi ya pekee katika maisha yao, hasa kutokana na mchango wake katika kuimarisha umoja na mshikamano wa familia.
Mungu ametwaa









